Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimewataka wenye kampuni na taasisi mbalimbali kupeleka wafanyakazi wake kupata mafunzo yatakayowawezesha kuboresha ujuzi wao sehemu za kazi.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Prof Edda Lwoga, akizungumza wakati wa mkutano na maofisa watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za fedha ulioandaliwa na chuo hicho kwaajili ya kufahamiana na kutoa maoni yao namna ya kuboresha chuo hicho.
Amesema chuo hicho kina uzoefu mkubwa wa kufanyakazi na sekta ya umma na sekta binafsi hivyo aliwahimiza kuwapeleka CBE kujifunza ili wapate ujuzi mbalimbali.
Amesema CBE ni chuo kikongwe kilichoanza mwaka 1965 na kilizinduliwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalim Julius Nyerere na mwaka 1983 walianzisha Kampasi yao mkoani Mwanza.
Amesema CBE imeendelea kutanuka kwa kuanzisha kampasi mbalimbali kwenye mikoa ya Dodoma na Mbeya na kwamba idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa nayo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Amesema mbali na CBE kuwa chuo cha kwanza kutoa elimu ya biashara nchini kimeendelea kutoa kozi adimu na kwasasa wanatoa pia kozi ya utalii ili kuunga mkono jitihada za serikali za kutangaza vivutio vya utalii nchini.
Amesema serikali imewekeza sana kwenye miundombinu ya elimu hivyo na chuo hicho kimejitahidi kuwekeza kwenye kutoa mafunzo ya vitendo yanayomwezesha mwanafunzi kujiajiri au kuajiriwa anapomaliza masomo.
“Tunatoa elimu ambayo inalenga kuibua mawazo ya biashara miongoni mwa wanafunzi wetuhali ambayo imewawezesha wengi wakimaliza chuo wajiajiri na waajiri wengine,” amesema
Amesema katia kujitanua zaidi CBE imeanza kufundisha shahada 10 za Uzamili kwenye kampasi zake za Dar es Salaam na Dodoma, Shahada ambazo zimejikita kwenye maeneo ya biashara, rasilimali watu na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Amewaomba wakuu hao wa kampuni na taasisi kupeleka wafanyakazi wao kwenye chuo hicho ili wawajengee uwezo wa kusaidia kukuza makampuni yao.
Amesema wanakozi mbalimbali ikiwemo ya ubora wa viwango, vipimo na mizani inayotolewa Dar es Salaam na kampasi ya Dodoma hivyo aliwataka wenye kampuni kuwapeleka wafanyakazi wao.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu