April 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CAG alivyoibua madudu mashirika ya umma

Na Joyce Kasiki,Dodoma

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Charles Kichere amewasilisha ripoti ya ukaguzi wa utendaji wa kifedha wa mashirika ya umma 217 kwa mwaka wa fedha wa 2023/24, ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita 2022/23 na kubaini mashirika ya umma 12 yalipata hasara ya kifedha kwa miaka mitatu mfululizo.

Aidha CAG Kichere amesema, mashirika matano yalipata hasara kwa miaka miwili mfululizo, wakati mashirika mawili yalipata hasara kwa mwaka wa 2023/24.

Pia ukaguzi huo umebaini mashirika ya umma 64 yalikabiliwa na ukata, yakiwa na madeni ya muda mfupi kuliko mali za muda mfupi kwa zaidi ya mwaka mmoja ambvapo miongoni mwao, mashirika ya umma ya biashara yalikuwa 14 , wakati mashirika ya umma yasiyo ya kibiashara yakiwa 50.

“Uwiano wa mashirika haya ulianzia 0.00 hadi 0.96 ikionesha upungufu wa kifedha na ukosefu wa ufanisi katika kusimamia fedha za muda mfupi. Zaidi ya hayo, nilibaini mashirika ya umma yasiyo ya kibiashara 28 yameendelea kupata nakisi kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na ukusanyaji mdogo wa mapato ya vyanzo vya ndani na utegemezi mkubwa wa ruzuku ya serikali na kuibua shaka kuhusu uendelevu wao wa kifedha.

CAG Kichere ameyasema hayo Aprili 16,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi mara baada ya kuwasilisha ripoti yake Bungeni.

Kichere alisema pia, alibaini  mashirika ya umma 11 yameshindwa kuchangia asilimia 15 ya mapato ghafi kwenda serikalini kama inavyotakiwa, kwa miaka miwili mfululizo, huku shirika moja likilimbikiza michango ambayo haijalipwa kwa zaidi ya miaka minne. Ufanisi wa Mashirika ya Umma Katika Kuimarisha Biashara.

Aidha alisema katika tathmini yake ya ufanisi wa uendeshaji wa mashirika ya umma ya biashara na ya kimkakati, alibaini Shirika la Reli Tanzania limeshindwa kufikia asilimia 61 ya mkakati wake wa usafirishaji wa shehena kwa wafanyabiashara wakubwa watano.

“Pia Shirika la Reli Tanzania limeshindwa kutoa huduma za usafiri kwa abiria katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa asilimia 72 kutokana na upungufu wa treni za kisasa zinazoendana na huduma hiyo .

Kichere pia alisema katika Kampuni ya ndege Tanzania, alibaini tozo za ukodishaji wa ndege na akiba ya matengenezo kwa miaka sita mfululizo yenye jumla ya shilingi bilioni 369.13 ambazo hazijalipwa, na matengenezo yasiyo na tija kiasi cha shilingi bilioni 20.63 ya Ndege-5H-MWF (Q300) ambayo ilikuwa haifanyi kazi.

Alisema,hadi kufikia 30 Juni 2024  imesababisha kampuni ya ndege Tanzania kupata hasara kubwa ya kifedha na kupunguza utendaji wake.

“Hatimaye, Kampuni ya Ndege Tanzania ilipata hasara ya shilingi bilioni 91.80 na kupunguza uwezo wa utendaji.”alisema

Vile vile alisema katika kampuni ya huduma za meli Tanzania ukaguzi wake ulibaini  miradi minne mikubwa, ambayo inahusisha ukarabati wa meli, ujenzi wa maeneo ya meli, na ujenzi wa gati katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria, ulikuwa haujaanza.

“Miradi hii ilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 8.89 na dola za Marekani milioni 251.07,usimamizi wa Mapato Katika Mashirika ya Umma Katika ukaguzi wangu nilibaini mashirika ya umma saba yalipata hasara ya shilingi milioni 966.42 itokanayo na mapato yasiyotozwa kwa kiwango sahihi,

“ Vilevile nilibaini upotevu wa mapato ya shilingi bilioni 6.97 kutokana na hali mbaya ya barabara ya Rongai na ukiukwaji wa mkataba wa ukodishaji katika Hifadhi za Taifa Tanzania . “

Katika hatua nyingine alisema,ukaguzi wake ulibaini utendaji duni wa Shirika la Madini la Taifa katika huduma ya uchimbaji, uliopelekea hasara ya mapato yaliyotarajiwa ya dola za Marekani milioni 15.52 sawa na shilingi bilioni 40.77.

Alisema,kwenye ukusanyaji wa mapato alibaini mapato yaliyokusanywa nje ya mfumo wa GePG shilingi bilioni 89.73 katika mashirika ya umma kumi  kati ya mashirika ya umma 217 aliyoyapitia mwaka 2023/24.

“ Hili ni ongezeko la shilingi bilioni 68.27 (sawa na asilimia 318) kutoka shilingi bilioni 21.46 zilizoripotiwa kwa mwaka uliopita,pamoja na hayo nilibaini mashirika ya umma 106 yana madai makubwa ya zaidi ya mwaka mmoja yanayofikia shilingi trilioni 3.58, yanayohusiana na huduma zilizotolewa kwa wateja. “alisema Kichere

Kichere ameongeza kuwa “Usimamizi wa Matumizi Katika Mashirika ya Umma nilibaini kuwa mashirika ya umma 12 yalifanya matumizi yasiyokuwa na tija ya jumla ya shilingi bilioni 371.42, hii ni ongezeko la asilimia 413 ikilinganishwa na shilingi bilioni 72.36 katika mashirika ya umma 17 mwaka uliopita. “

Vilevile, nilibaini kuwa mashirika 10 yalifanya matumizi yasiyostahili ya jumla ya shilingi bilioni 6.75, ikiwa ni ongezeko la asilimia 45 ikilinganishwa na shilingi bilioni 4.64 katika mashirika ya umma 11 mwaka uliopita. Vilevile alisema , ukaguzi wake  ulibaini kuwa mashirika 66 ya umma yalikuwa na madeni ya jumla ya shilingi trilioni 3.70, ambayo yalikuwa hayajalipwa kwa zaidi ya miezi 12.

“Usimamizi wa Bajeti Katika Mashirika ya Umma Nilibaini Serikali haikutoa shilingi bilioni 485.91 kwa mashirika ya Umma 66 kama ilivyopangwa katika mwaka wa fedha 2023/24. Aidha, kwa kipindi cha mwaka wa 2022/23, Serikali haikutoa shilingi trilioni 1.01 kwa mashirika 50.”

 Vilevile, nilibaini mashirika ya umma 80 hayakukusanya fedha kiasi cha shilingi trilioni 2.07 kutoka katika bajeti ya vyanzo vya ndani katika mwaka wa fedha 2023/24.

Aidha alisema, kwa kipindi cha mwaka wa 2022/23, mashirika ya umma 66 hayakukusanya fedha kiasi cha shilingi bilioni 284.71 kutoka katika bajeti ya vyanzo vya ndani.

Lakini pia alisema,alibaini mashirika ya umma 12 yalitumia zaidi ya bajeti kwa kiasi cha shilingi bilioni 7.65 bila idhini ya afisa masuuli au Bodi ya Wakurugenzi, na kwamba kwa mwaka wa fedha 2022/23, aliripoti mashirika ya umma nane kati ya mashirika 215 yalitumia zaidi ya bajeti kwa kiasi cha shilingi bilioni 21.14 bila idhini ya Afisa Masuuli au Bodi ya Wakurugenzi.