December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BUWSSA kuondoa mita chakavu 6000 kuthibiti upotevu wa maji

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MAMLAKA ya Majisafi na usafi wa mazingira Bunda (BUWSSA)imeweka mkakati wa kubadilisha na kuziondoa mita goi goi(mitachakavu)6000 zilizokaa zaidi ya miaka 10 ili kumaliza na kudhibiti tatizo la upotevu wa maji.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Julai 20 ,2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo,Esther Gilyoma wakati akizungumza na waandishi habari kuhusu utendaji kazi na muelekeo wa kufikia asilimia 95 ya huduma ya maji Mjini Bunda kwa mwaka 2025.

Gilyoma amesema kuwa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bunda inatumia maji toka chanzo cha ziwa Victoria, chanzo hicho ni cha uhakika kiko eneo la Nyabehu umbali wa Km 24.8 toka Bunda Mjini.Chanzo hicho kina uwezo wa kuzalisha maji lita 4000 huku mahitaji yakiwa lita 9857 huku upotevu wa maji ukiwa ni asilimia 36 kutokana na uchakavu wa mita za maji.

Amesema kuwa Upotevu wa maji hasa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ni asilimia 36 Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Bunda imeweka mikakati ya kupunguza upotevu wa maji ulioandaliwa ikiwa ni mpango mkakati wa kupunguza upotevu wa maji wa miaka mitatu ulioanza mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2023/2024 unaoendana na mpango wa kibiashara wa Mamlaka ya maji.

Hivyo amesema Mamlaka hiyo imeandaa andiko mradi kwa ajili ya kukopa fedha kiasi cha shilingi 815,000,0000 mfuko wa maji ili kuhakikisha upotevu wa maji unapungua kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024.

“Mita zetu ni chakavu zimekaa zaidi miaka 10 hadi 15 lazima tuzibadilishe natuna uhakika wa kupata fedha ya mkopo milioni 800 hivyo tutazibadilisha ili kudhibiti tatizo hili kwani mwanzo upotevu ulikuwa asilimia 45 hivyo tulijitahidi kupunguza na kwasasa tutakarabati hadi 2025 tutakuwa tumedhibiti kwa asilimia 15,”amesema.

Pia amesema kuwa kwa sasa BUWASA haina
huduma ya majitaka,hivyo magari ya watu binafsi ambayo yanasimamiwa na Halmashauri ya mji wa Bunda ndiyo yanatumika katika kutoa huduma za majitaka.

Kutokana na hilo Gilyoma amesema kuwa kupitia Mamlaka ya maji Bunda kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wanategemea kuanza kujenga miundo mbinu ya majitaka eneo la Butakale liliyoko Mjini Bunda.

Aidha amesema kuwa Mamlaka hiyo ina chujio la kutibu maji (Convertion treatment plant) liliyoko eneo la Nyabehu,kupitia chujio hilo maji yamekuwa yakitibiwa kwa kutumia dawa zifuatazo,Poly-Aluminum Chloride (PAC)Calcium hypochlorite ambayo inawafanya wananchi wa Bunda kupata maji safi na salama.

Amesema pamoja na mipango tajwa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Bunda imeomba kuongezewa eneo la utendaji la Mamlaka ya majisafi na usafiwa mazingira Busega,Kibara na Nyamswa nia ikiwa ni kuboresha huduma, kuongeza idadi ya wateja ambao watasaidia kupunguza gharama za uendeshaji na kupunguza gharama ya bili ya maji.

Pia ametoa rai kwa Wananchi wa Bunda kuendelea kulinda miundo mbinu ili iwatunze maji kwani maji ni uhai na hayana mbadala.