November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bustani ya wanyama Luhila kuboreshwa

Na Cresensia Kapinga, Timesmajira,Online Songea

MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA) Meja Jenelari Mstaafu, Hamis Semfuko amesema wameweka mikakati ya kuboresha bustani ya wanyama pori wapole na wakali katika bustani iliyopo Luhila Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma.

Amesema tayari wanyama kama Pundamilia, nyumbu pamoja na kongoni wanaongezwa katika bustani hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kumaliza kikao cha Bodi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TANESCO Manispaa ya Songea, alisema lengo la ziara hiyo ni kuboresha maeneo ya bustani ya wanyama Pori ili wananchi wa maeneo mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo waweze kufika na kujifunza mambo mbalimbali ya utalii.

Amesema tayari wametenga kiasi cha fedha sh. milioni 100 ili kujenga sehemu ya kuhifadhia wanyama wakali kama Simba, Chui ambao wanatarajiwa kuletwa kwenye bustani hiyo na kuongeza mapoto.

“Wanahabari tumetembelea hapa Luhila kwa lengo kuongeza wanayama wapole na wakali ili eneo hili liwe kitovu cha wanyama kama chui, Simba, Twiga na wengine, nafahamu kuwa wanyama wakiongezeka watu watakuja kutalii na hivyo tutaweza kuongeza mapato,”amesema Meja Jenelari Semfuko.

Ametoa agizo atafutwe mwekezaji binafsi, kampuni ama shirika ili waweze kuwekeza katika eneo hilo kwa kujenga hoteli, baa na sehemu za kufanyia mazoezi kwa lengo la kufanya utalii wa ndani kwa kutumia baskeli na wao wanaanza kwa kuboresha sehemu za kupumzikia na kuchezea watoto.

Aidha ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na maeneo mengine nchini kutembelea vivutio vilivyopo nchini ikiwemo Luhila.

Kwa upande wake Kamnda wa Kikosi dhidi ya Ujangili na Mkuu wa Kituo cha Luhila, Keneth Sanga amesema kuwa kwa mwezi wanapata watalii wanaotembelea kwenye bustani hiyo 30 hadi 40 kwa mwaka 200 mpaka 300, hivyo wamejipanga kuongeza idadi ya watalii kufikia 5,000 kwa mwaka na watalii wanaopenda kutembelea busatani hiyo ni kutoka ndani ya nchi na nje ya nchi.

Amesema wanatarajiwa kuanzisha utalii wa kuangalia nyoka kwa lengo la kuwavutia zaidi wananchi wanaopenda kuangali chatu na aina nyingine za nyoka.

Bustani ya wanyama Pori Luhila ina eneo la kilometa tatu za mraba ambazo zimezungushiwa uzio na kwamba ilianzishwa mwaka 1973.