December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bunge lataka tija uwekezaji soko jipya la Kariakoo

Na. Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Denis Rondo amelitaka shirika la Masoko ya Kariakoo (KMC) kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali kwa kutoa shilingi Bilioni 28.03 kukarabati na kujenga soko la Kariakoo unakuwa na tija kwa taifa na kuwezesha wafanyabiashara kuwa na mazingira mazuri kuchangia ukuaji wa uchumi.

Hayo yamebainishwa leo ( Agosti 22,2023) bungeni jijini Dodoma wakati Kamati hiyo ya Bunge ilipokutana na Menejimenti ya Shirika la Masoko ya Kariakoo kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za shirika hilo kwa mwaka 2022/23.

Rondo ameitaka pia Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia idara ya miundombinu kusimamia kwa ukaribu miundombinu ya soko la Kariakoo ili thamani ya fedha iliyowekwa na serikali iweze kuonekana.

” Idara ya miundombinu TAMISEMI isimamie miundombinu ya masoko ili shilingi Bilioni 28 za serikali iwe na tija kwa Nchi” alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Deo Ndejembi alisema katika kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya awamu ya sita kwenye ,Shirika la Masoko ya Kariakoo litaanza kutumia mfumo wa kielektoniki wa TAUSI katika kusajili na kutoa leseni kwa wafanyabiashara tofauti na ilivyokuwa awali.

Ndejembi aliongeza kusema kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI itashirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wadogo kwenye soko la Kariakoo na masoko mengine nchini ili wafanye kazi zao kwa utulivu na hivyo kuchangia pato la taifa na kuepukana na migogoro.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo Sigsibert Valentine alisema mradi wa ukarabati na ujenzi wa soko la Kariakoo ulioanza Mwaka 2022 unatarajia kukamilika mwezi Oktoba 2023 na kuwa shirika liko kwenye maandalizi ya kuwarejesha waliokuwa wafanyabiashara kabla ya soko kuungua na kuweka mfumo utakaotumika kuingiza wafanyabiashara wapya kutokana na nafasi za biashara kuongezeka toka 1’660 hadi takribani 2,300.