January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bumbuli DC yavuka lengo ukusanyaji mapato ya ndani

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Bumbuli

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Ameir Sheiza amesema halmashauri hiyo imevunja rekodi kwa ukusanyaji wa Mapato ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2023/2024 baada ya kukusanya sh. 1,149,000,000 ikiwa ni sawa na asilimia 102 ya mapato hayo.

Na kummwagia sifa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Baraka Zikatimu kuwa ujio wake wa kurudi tena kama Mkurugenzi, ndiyo aliyefanya mageuzi katika ukusanyaji wa mapato hayo. Miaka ya nyuma, Zikatimu alikuwa halmashauri hiyo kama Mkuu wa Idara ya Mipango.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo robo ya nne, ambapo alisema kwa sasa halmashauri hiyo inakwenda vizuri katika ukusanyaji wa mapato, ambayo yatawasaidia kuweza kupanga shughuli za miradi ya maendeleo ya wananchi.

“Kwa mwaka wa fedha 2023/2024, halmashauri yetu imeweza kuvuka lengo la ukusanyaji mapato kwa kuweza kukusanya asilimia 102 ya mapato hayo. Kazi kubwa imefanywa na Mkurugenzi wetu (Baraka Zikatimu). Tunaendelea vizuri katika ukusanyaji mapato, na tunataka kazi hii ya ukusanya mapato iweze kuendelea ili kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi” alisema Sheiza.

Akijibu hoja za madiwani akiwemo Diwani wa Kata ya Dule B Ali Mkwavingwa  kuhusu fedha za miradi ya maendeleo kutengwa kutoka kwenye Mapato ya Ndani, Mkurugenzi Mtendaji, Zikatimu amesema fedha hizo zimetengwa kwa asilimia 100 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, na zile asilimia 10 ya Mapato ya Ndani za vikundi kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Zikatimu amesema halmashauri hiyo ni miongoni mwa halmashauri 10 nchini ambazo zimechaguliwa kuanza kutoa fedha za mikopo kupitia kwenye mabenki kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kwasasa wanasubiri Mwongozo kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuanza kutoa fedha hizo zinazotokana na Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa walengwa.

“Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli iliidhinishiwa na Baraza la Madiwani kukusanya sh. 1,122,613,000, lakini iliweza kukusanya sh. 1,149,000,000 sawa na asilimia 102. Sasa katika fedha hizi, sisi tupo kwenye kundi la kuchangia asilimia 20 (miradi ya maendeleo) kwenye Mapato ya Ndani, ndiyo ile milioni 162 aliyokuwa anaihoji Mjumbe (Mkwavingwa). Katika fedha zile, kuna asilimia 10 zinatengwa kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Na fedha hiyo tumeshaitenga kwa asilimia 100 na ipo na hiyo ni component (sehemu) ya aliyokuwa anahoji Mjumbe.

“Kwa hiyo, zile fedha zipo na tukishapata Mwongozo tunazitoa,lakini pia kuna fedha tulizipeleka kwenye jengo letu la Nanenane (Morogoro)mara ya kwanza tulipeleka sh. milioni 10 lile jengo limekamilika na ninyi (madiwani) mlikwenda mmeona, na juzi tumetoa sh. milioni tatu kwa ajili ya kukamilisha huduma za choo. Lakini pia tumetoa sh. milioni nane (8) kwa ajili ya vibanda vya Soni vya biashara, pia kuna milioni 43 hazijatumika sababu ya Mfumo, na nimetaja hizo fedha kubwa”amesema Zikatimu.

Zikatimu amesema, katika suala la kuimarisha mapato Stendi Kuu ya Mabasi Soni, watahakikisha wanashirikiana na vyombo vingine kama polisi wa usalama barabarani ili kuona mapato hayo hayapotei ni baada ya kuelezwa na baadhi ya madiwani kuwa baadhi ya mabasi makubwa na madogo, hayaingii kwenye stendi hiyo, hivyo kuipotezea mapato halmashauri hiyo.