January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bugando yakamilisha ukarabati wa ujenzi ICU kwa asilimia 100, kupitia fedha za Uviko-19

-Yatumia bilioni 3.9 fedha walizopokea kati ya bilioni 4.2 zilizotengwa na serikali
-Jumla ICU itakuwa na vitanda 51

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Katika kuhakikisha maisha ya watanzania yanaokolewa,Serikali ilitenga kiasi cha bilioni 4.2 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) na ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

Hadi sasa hospitali ya Bugando imesha pokea kiasi cha bilioni 3.9 ambacho kimetumika katika ukarabati na ununuzi wa vifaa ambapo kwa upande wa ukarabati umekamilika kwa asilimia 100 huku vifaa tiba imekamilika kwa asilimia 90.

Akizungumza katika sherehe ya upokeaji wa vifaa tiba na upanuzi wa chumba cha wagonjwa mahututi, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt.Fabian Massaga, ameleeza kuwa baada ya nchi kupitia changamoto ya Uviko-19 mwaka 2021.

Rais kwa juhudi zake aliweza kutafuta fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utoaji huduma za afya hasa katika huduma za magonjwa mahututi na dharura kupitia fedha za Uviko-19 zilizofadhiliwa na mfuko wa IMF Bugando imekuwa moja ya mnufaika wa fedha hizo.

Dkt.Massaga ameeleza kuwa Bugando ilitengewa jumla ya bilioni 4.2 na mpaka sasa wamepokea bilioni 3.9 ikiwa ni kwa ajili ya ukarabati wa ICU na ununuzi wa vifaa tiba na fedha iliobaki Wizara inakamilisha mchakato wa kuwanunulia gari la kisasa la kubebea wagonjwa na gari maalumu la kuhifadhia na kusafirishwa damu.

Ameeleza kuwa ukarabati wa ujenzi wa ICU umekamilika kwa asilimia 100, na umegharimu kiasi cha milioni 500,vifaa tiba vya ICU milioni 900, vifaa tiba vya EMD milioni 800,Echocardiography machine milioni 115,apheresis machine milioni 150,telemedicine milioni 181, mtambo wa oxygen plant milioni 658 na oxygen plant ujenzi wa miundombinu.

“Ujenzi umejumuisha upanuzi wa ICU ya magonjwa ya ndani(medical),magonjwa ya upasuaji(surgical) na magonjwa ya watoto wachanga(neonatal),kabla ya maboresho tulikuwa na ICU yenye vitanda 12 kwa magonjwa yote ya ndani na upasuaji na vitanda 12 kwa watoto wachanga ila sasa hivi tutakuwa na ICU yenye jumla ya vitanda 51(medical 11, surgical 19 na neonatal 21 na ujenzi umekamilika kwa asilimia 100 huku vifaa ni asilimia 90,”ameeleza Dkt.Masaga.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,ameeleza kuwa vifaa vilivyowekwa ni vya kibobezi hivyo ameutaka uongozi wa hospitali hiyo pamoja madaktari na wauguzi watoe huduma kwa kutafsiri ubobezi wa vifaa hivyo kwa vitendo katika kuwahudumia Watanzania.

Mhandisi Gabriel,ameeleza kupitia maboresho hayo changamoto walizokuwa wanapata wananchi za kupata huduma za kibobezi kuzifuata Dar na maeneo mengine sasa zinapatika katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

“Nimapinduzi makubwa katika sekta ya afya na zaidi katika kutokomeza vifo vinavyotokana na magonjwa mbalimbali,tumeshuhudia kuanza kwa huduma za kibobezi kwa ajili ya huduma za dharura na mahututi na kazi zimeanza,”ameeleza Mhandisi Gabriel.

Kwa upande wake Muuguzi Kiongozi idara ya wagonjwa mahututi ya watoto wachanga(Neonatal Intensive Care Unit) hospitali ya Bugando Sophia Sembe,ameeleza kuwa wameweza kupata jengo bora na zuri zaidi ambapo kwa sasa wanaweza kuhudumia wagonjwa wengi zaidi ambapo mwanzoni hatukuweza.

“Kwa sasa tunaweza kuwahudumia wagonjwa 21 kwa wakati mmoja wakati awali tuliweza kuhudumia wagonjwa 10,lakini kwa jengo bora na huduma bora tunahitaji rasilimali watu,tunahitaji timu ya wauguzi wa kutosha na madaktari wabobezi ili tuweze kutoa huduma bora zaidi,tunaimani Serikali itafanyika kazi,”ameeleza Sembe.

Naye Daktari Bingwa Kitengo cha Sikoseli Dkt.Emmanuela Ambrose,ameeleza kuwa kwa upande wa Kanda ya Ziwa mashine hiyo ya Apheresis ambayo inafanya kazi ya kutenganisha damu na viambata vya damu itafanya kazi sana kwenye sikoseli na saratani ambayo ipo zaidi katika ukanda huo.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt.Fabian Massaga kushoto akimuelezea Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,kulia juu ya namna utekelezaji wa ujenzi wa upanuzi wa jengoa ICU na dharura pamoja na ununuzi wa vifaa tiba ulivyofanyika,kabla ya Mkuu huyo wa Mkoa kukataa utepe katika sherehe ya upokeaji wa vifaa tiba na upanuzi wa ICU ilifanyika hospitalini hapo.(Picha na Judith Ferdinand)
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, akizungumza katika sherehe ya upokeaji wa vifaa tiba na upanuzi wa ICU katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ilifanyika hospitalini hapo.(Picha na Judith Ferdinand)
Muonekano wa ICU zilizofanyiwa ukarabati katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,akikataa utepe katika sherehe ya upokeaji wa vifaa tiba na upanuzi wa ICU hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ilifanyika hospitalini hapo.(Picha na Judith Ferdinand)
Mashine ya Apheresis ambayo itafanya kazi ya kutenganisha damu na viambata vya damu katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.