Na Cresensia Kapinga, TimesmajiraOline, Songea
BRUDA wa Shirika la Kimisionari la Benedictine Father’s Peramiho, Kizito Nsafiri OSB, ametembea kwa miguu umbali wa kilometa 275 kutoka mkoani Njombe hadi Peramiho, mkoani Ruvuma ili kukamilisha Hija yake ya kuliombea Jimbo la Njombe liweze kupata askofu mpya.
Jimbo la Njombe halina askofu tangu mwaka 2021 baada ya askofu aliyekuwa akiongoza jimbo hilo kufariki kwa ajali ya gari.
Bruda huyo kutoka kwenye Shirika hilo lilipo Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, aliwaambia waandishi wa habari jana kwenye viwanja vya Kanisa la Peramiho ambako Hija yake ya kutembea kwa mguu aliikamilisha ndani ya siku nne, kwamba;
“Nilikuwa natembea kilometa 52 kwa siku nikiwa nimebeba mzigo wa kilo 10 ambao ndani yake ulikuwa na maji na biskuti.”
Amesema Hija yake ilikuwa na malengo matatu, lengo la kwanza lilikuwa ni kwa ajili ya kuungana na waumini wa Jimbo la Njombe ambao hadi sasa hawana askofu.
“Kwa hiyo kwamuda wote waumini wapo katika maombi ya kuomba wapate askofu mpya na si vinginevyo,” amesema. Kwa sasa askafu anayekaimu uongozi wa jimbo hilo ni Askofu John Ndimbo kutoka Jimbo la Mbinga.
“Kwa hiyo niliona nifanye Hija ambayo nitaomba watu mbalimbali bila kujali dini zao wanichangie pesa kiasi chochote na kila nitakachokipata nitakiwakilisha jimboni ili kutayarisha maandalizi ya Askofu mpya ili atakapoteuliwa ataziwasilisha ili zitumike katika shughuli zitakazoandaliwa,” amasema Bruda Kizito.
Alisema anamshukuru Mungu, kwani kila aliyemshirikisha na wengine waliosikia wamempigia simu wakiomba katika safari ya kukutana na Mungu kwenye Hija.
Ametaja lengo la pili katika hija yake kwamba ilikuwa ni kuiombea nchi amani na utulivu na kumuweka kwenye maombi Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ili Mwenyezi Mungu amuepushe na wale wote wenye nia mbaya na nchi, ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Aidha, amesema lengo la tatu ilikuwa ni la kuombea watawa na mapadre ili wadumishe upendo wao kwa wao.
Akieleza changamoto kubwa aliyokutanana nayo kwenye safari yake hiyo ya kilometa 275, alisema ni miteremko mikali jambo ambalo lilikuwa linamchosha.
“Nimekutana na Nyoka, lakini namshukuru Mungu sikukutana na wanyama wakali licha ya kuwepo kwa misitu mikubwa ya kutosha,”amesema Bruda huyo.
Kwa upande wao Watawa wenzake walimpongeza kwa kitendo cha kufanya Hija na kutembea zaidi ya kilometa 275 kwa miguu amedhihirisha kuwa Waseminari walikuwa wanaeneza Injiri kwa kutembea umbali mrefu.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba