December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BRELA yapeperusha bendera ya Tanzania, mkutano mkuu wa ARIPO

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Tanzania inashiriki katika Mkutano wa 46 wa Baraza la Uongozi la Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (ARIPO), kujadili taarifa mbalimbali za utendaji kazi wa ARIPO  na kupitia taarifa mbalimbali za Itifaki zinazosimamiwa na ARIPO

Mkutano huo  ulioanza rasmi  Novemba 21, 2022 Maputo, Msumbiji, unahudhuriwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),  Godfrey Nyaisa, Afisa,  Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA),  Mariam Jecha ,Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu Seka Kasera pamoja na mwakilishi kutoka ofisi ya  Hakimiliki Tanzania  Philimon Kilaka.

Taarifa iliyotolewa na Wakala wa BRELA imesema  Brela  ni Ofisi ya Miliki Ubunifu nchini na imekuwa mshiriki mkubwa wa  ARIPO kwenye masuala mbalimbali yanayohusu Miliki Ubunifu kwenye Ukanda wa Afrika. 

“Katika Mkutano huo masuala mbalimbali yatajadiliwa hasa kuhusu Hataza, Maumbo Bunifu, Alama za Biashara na Huduma, Hakimiliki na linzi zingine za Miliki Ubunifu,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Mkutano huo wa siku tano utakaohitimishwa Novemba 25, 2022 umefunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Msumbiji, Silvino Mareno na takribani nchi wanachama 22 wa ARIPO  zinashiriki ikiwa ni pamoja na WIPO  na mashirika mengine ya kikanda na kimataifa.