December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Brela yajinyakulia tuzo tatu maonesho ya Sabasaba 2023

Na Penina Malundo,Dar es Salaam

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeibuka kidedea kipengele cha Banda Bora ndani ya Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam yaliyofanyika katika uwanja wa Mwalimu J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam na kujizolea tuzo tatu katika maonesho hayo.

Akizungumza jana,Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Brela,Andrew Mkapa wakati akiongea na waandishi wa habari baada ya kupokea tuzo hizo kutoka kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Mwinyi, wakati wa kufunga maonesho hayo.

Amesema tuzo hizo wamepata katika vipengele vitatu tofauti ikiwemo Tuzo ya udhamini wa Taasisi za serikali katika maonesho hayo,tuzo ya uwekezaji na uwezeshaji wa Ukuzaji wa Biashara na tuzo ya mwisho waliyopata ni ya Banda bora katika mabanda yote ambayo yameshiriki maonesho hayo ya Sabasaba Mwaka huu.

“Nishukuru wafanyakazi wote wa brela kwa kupokea tuzo hizi zote kwani zimepatikana kwa sababu ya michango yao, hauwezi kupata mtu mmoja ni kwamba ukiunganisha nguvu za watumishi wote matokeo yake ni haya,amesema na kuongeza

“Nawashuku na nawapongeza tuendelee kufanya hivi hata katika maonesho yajao ili tuweze kuonesha umahiri wetu katika ushiriki wa Sabasaba,”amesema

Ushindi wa nafasi ya kwanza kwa BRELA ni mwendelezo wa jitihada za Taasisi katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja na wadau wake, ambapo katika Maonesho ya 46 BRELA ilipata ushindi wa nafasi ya pili katika kipengele hicho hicho cha Uwezeshaji wa ukuzaji wa Biashara na Uwekezaji.

Kabla ya kufunga Maonesho hayo, Rais Mwinyi alitembelea Banda la BRELA ambapo alipata fursa ya kuona jinsi Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS) unavyofanya kazi. Pia alitumia nafasi hiyo kukabidhi Cheti cha Usajili kwa mmoja wa wafanyabiashara waliofika katika Banda la BRELA na kupata huduma ya usajili wa papo kwa papo zilizotolewa wakati wa Maonesho hayo kiwanjani hapo.