Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
WAKALA wa Biashara na Leseni (BRELA) imeadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutembelea wagonjwa katika Hospitali ya Amana, kufanya usafi na kuwapatia elimu juu ya huduma za Usajili wa Biashara na Leseni kwa wafanyabiashara katika soko la Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo ilianza Juni 16 na kilele chake kufikia Juni 23.
Ambapo Wizara na taasisi zake zinatakiwa kutoa huduma kwa wadau wake na wananchi kwa ujumla kutokana na michango wanayoitoa kwa Serikali yao.
Wakiwa katika Hospitali ya Amana, Watumishi wa BRELA walikabidhi mahitaji mbalimbali ya wagonjwa ikiwa ni pamoja na Sabuni, Taulo za Kike (Pads) na Daipers za watoto na wakubwa.
Pia walitumia fursa hiyo kuchangia damu. Mkuu wa Kitengo cha Uhusuano kutoka BRELA, Roida Andusamile akizungumza wakati wa kukabidhi bidhaa hizo amesema taasisi hiyo pamoja wa kuwezesha biashara kwa kusajili Majina ya Biashara, Kampuni, Alama za Biashara na Huduma, utoaji wa Leseni za Biashara kundi A na Leseni za Viwanda na Hataza, inajali jamii inayoizunguka kwa kuwapatia msaada pindi fursa inapopatikana.
“BRELA imefika hospitali ya Amana na kuchangia mahitaji ya msingi ya wazazi na watoto ili wanapoendelea na matibabu wawe katika hali ya usafi,” alifafanua, Andusamile na kuongeza kuwa utaratibu huu utaendelea kufanyika katika hospitali mbalimbali za hapa nchini.
Akipokea msaada huo, Daktari Bingwa wa magonjwa ya kinamama Dkt. Baya Kissiwa ameishukuru BRELA kwa msaada iliyo utoa kwa wagonjwa na kutoa wito kwa taasisi zingine kufika hospitalini hapo na kuwasaidia wagonjwa.
Dkt. Bingwa amesema kuwa hospitali hiyo kwa sasa ina uhitaji mkubwa wa damu hasa kwa wazazi wanaofika hospitalini hapo kwa matibabu, hivyo inawaomba wananchi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Aidha katika soko la Kisutu, watumishi wa BRELA walitoa elimu kwa wafanyabiashara na kuwahimiza kufanya sajili za biashara ili kuzipa utu wa kisheria biashara zao.
Pamoja na kutoa elimu sokoni hapo, Watumishi wa BRELA walifanya usafi ndani ya soko hilo, ikiwa ni moja ya jukumu la watumishi wa umma kuwajibika kwa wananchi.
Awali Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Seka Kasela ametumia Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kuwahudumia wateja waliofika katika ofisi za BRELA kupata huduma mbalimbali.
Maadhimisho haya yanaoyoratibiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora yalifanyika sambamba na kaulimbiu “Kujenga Afrika tunayoitaka, kupitia utamaduni wa uadilifu ambao unastawisha uongozi wenye maono hata katika mazingira ya mgogoro.”
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi