Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DSM
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni, (BRELA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) yasaini hati ya makubaliano ya utendaji kazi kwa lengo la kurahisisha na kuharakisha taratibu mbalimbali za kiuchunguzi bila kuathiri Mamlaka na Mipaka ya kiutendaji kati ya taasisi hizi mbili.
Hafla fupi ya utiaji saini ya hati ya makubaliano kati ya BRELA na TAKUKURU yameongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Godfrey Nyaisa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), CP. Salum Hamduni leo tarehe 7 Desemba, 2023 katika ofisi ya makao makuu ya BRELA jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Nyaisa amesema kuwa Makubaliano hayo ni kuona uchunguzi unaenda kwa wakati na kuhakikisha TAKUKURU wanapata taarifa zilizo sahihi na mahiri kwa wakati huku tukibainisha changamoto zilizopo katika utendaji kazi baina ya BRELA na TAKUKURU na kupendekeza kwa pamoja ufumbuzi wake
“Katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku BRELA imekuwa ikipokea barua si chini ya sita (6) kwa siku kutoka TAKUKURU zinazohitaji taarifa za usajili wa kampuni mbalimbali, pia tumekuwa tukipokea wito mbalimbali zinazowahitaji Maafisa wa BRELA kwa ajili ya mahojiano TAKUKURU pamoja na kuhudhuria mahakamani kushuhudia taarifa za kumbukumbu hizo” amesema Bw Nyaisa.
Aidha, CP. Salum Hamduni ameeleza kuwa Mkataba huu utakaosainiwa unalenga kutia nguvu na kurasimisha ushirikiano wa taasisi mbili kwa maeneo yaliyokubaliwa na pande zote ambazo ni kubadilishana taarifa za kiuchunguzi kati ya taasisi hizi kwa lengo la kupata ushahidi utakowezesha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, kuimarisha mfumo na utaratibu wa Mafunzo kwa watumishi wa BRELA kuhusu dhana ya Rushwa, madhara yake na namna watumishi hao wanavyoweza kupambana na rushwa ndani ya BRELA na kushirikiana katika kufanya utafiti na tathmini ya mifumo ya kiutendaji ndani ya BRELA kwa lengo la kubaini na kuziba mianya ya rushwa ndani ya BRELA.
“Kwa kutambua kuwa rushwa ni Adui wa Haki, Utawala wa Sheria, Demokrasia na Maendeleo, Serikali imedhamiria kupambana na tatizo la rushwa kwa nguvu zote. Aidha, kwa kutambua kuwa mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila ushiriki wa wadau, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, imekuwa ikishirikisha wadau kwa namna mbalimbali ikiwemo kuingia nao mikataba ya ushirikiano” amesisitiza CP Hamduni.
CP Hamduni ameongeza kwa kusema kuwa TAKUKURU itauzingatia mkataba huu kuwa mojawapo ya nyenzo muhimu katika kuifikia ndoto (vision) ya Taasisi inayosema “Tanzania isiyokuwa na rushwa”, kama ambavyo inabainishwa katika Mpango Mkakati wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa Mwaka 2022/23 – 2025/26.
Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 8 hadi 9 Julai, 2022 BRELA na TAKUKURU ilikuwa na kikao kazi cha pamoja mkoani Morogoro chenye lengo la kupeana elimu ya kiutendaji ili kuleta mahusiano yenye tija katika kutimiza majukumu na kupeana taarifa mbalimbali kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria.
Kutokana na hilo ilionekana kuna umuhimu kwa Taasisi hizi kuanzisha utaratibu wa kuwa na vikao vya pamoja kwa lengo la kupeana elimu na uelewa kuhusu utendaji kazi wa majukumu ya Taasisi hizi, mafanikio na maboresho katika utendaji kazi kipekee katika usajili wa kampuni na biashara, utunzaji wa rekodi na taratibu za kufuata baada ya usajili, kubadilishana uzoefu pamoja na kubainisha changamoto mbalimbali ili kupata ufumbuzi wa pamoja kwa manufaa ya Taasisi hizi mbili
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu