November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BRELA kuanza kuwapa nembo ya utambulisho wakulima


Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WAKALA Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA)imesema ili kuwasaidia wakulima kusajili biashara zao rasmi umejipanga kuanza kuwasajili ili kuwapa nembo itakayo watambilisha.

Hayo yameelezwa leo Agosti 4,2024 kwenye maonesho ya Wakulima Nanenane Jijini hapa na 
Afisa usajili wa BRELA Gabriel Gilangay wakati akizungumza na Waandishi wa habari na kueleza kuwa Wakala huo unashughulikia mambo mengi  kwa wakulima nchini ikiwemo Usajili wa Biashara.

Amesema BRELA inawasaidia wakulima kusajili biashara zao rasmi ili  kuwa na usajili wa kampuni, ushirika, au biashara ndogo ndogo zinazohusiana na kilimo.

“Usajili huu unasaidia kupata haki ya kufanya biashara na kufanya biashara kwa ufanisi zaidi,usajili wa alama za Biashara ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za kusajili alama za biashara (trademarks) ambazo zinaweza kuwa muhimu kwa wakulima kulinda jina la bidhaa zao na alama zinazotumika katika masoko na kutoa Leseni na Vibali,”amesema

Mbali na hayo amesema  BRELA hutoa huduma hizo ili kuhakikisha  biashara za kilimo zinakubalika kisheria ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za ushauri kuhusu jinsi ya kufuata taratibu za kisheria katika biashara ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kanuni za usajili, sheria za biashara, na masharti ya leseni.

“Kwa hivyo, BRELA inachangia katika kuhakikisha kuwa wakulima wanapata huduma zinazohitajika ili kuendesha shughuli zao za kilimo kwa njia rasmi na kisheria, ” amefafanua Afisa usajili huyo.

Kwa upande mwingine Wakala huo hushughulikia Kampuni za Umma,Kampuni zinazoshiriki soko la hisa,Kampuni za Kibinafsi na Kampuni zinazomilikiwa na watu wachache.

“Kwa wakulima na wafanyabiashara wote hakikisheni  mmefanya utafiti wa kina kuhusu kampuni unayotaka kuisajili,angalieni pia Kampuni mnazotaka kuingia ubia nayo,angalia historia yake, hali ya kifedha, na sifa zake,” Amesema

Kuhusu kufanya Mkataba wa Ubia amesema mkataba wa ubia unaoeleza masharti ya ushirikiano unapaswa kuandaliwa mapema ikiwa ni pamoja na majukumu ya kila upande, na uwajibikaji.

Amesema, “Mkataba huu unapaswa kuwa wa kisheria na unaweza kuwa na huduma za kisheria kuhusiana na mgogoro wa baadaye.Kusajili na Kuandikisha: Hakikisha kuwa ubia wako umeandikishwa rasmi na BRELA au mamlaka husika.

“Ili biashara ifanyike bila usumbufu fahamu majukumu yako ya kisheria na yale yanayohusu ubia,hii ni pamoja na kutambua jinsi ya kulipa kodi, leseni, na vibali vya biashara lakini pia  mfumo mzuri wa mawasiliano na usimamizi wa mahusiano ya kibiashara unapaswa kuzingatiwa ili kuondoa migogoro na kuboresha ushirikiano,”amesema.