Na Mwandishi Wetu Timesmajira Online
BENKI Kuu ya Tanzania (BOT), imetangaza kuhamisha mali na madeni ya Benki ya Biashara ya China kwenda Benki ya Taifa ya NMB, baada ya benki hiyo kuwa na mtaji mdogo ambao usingeiwezesha benki kujiendesha vizuri katika kuhudumia wateja wake.
Akitangaza uamuzi huo leo jijini Dar es Salaam, Gavana wa BoT, Profesa Florence Luoga. Amesema kabla ya benki hiyo kuwekwa chini ya usimamizi wake, BoT ilifanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuitaka kuongeza mtaji kufikia kiwango kilichoitajika kisheria, lakini ilishindwa kufikia kiwango hicho.
“Kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 58(2)(h) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu imeamua kuhamisha kwa mujibu wa sheria (acquisition by operation of the law) mali na madeni ya China Commercial Bank kwenda NMB Bank Plc” amesema Prof.Luoga.
Prof. Luoga ameongeza kuwa BoT, NMB pamoja na wadau wengine wanaendelea kuandaa taratibu za kisheria za kukamilisha mchakato wa uhamishaji wa mali na madeni ya Benki ya Biashara ya China.
Hata hivyo, Prof.Luoga amesema BoT itaendela kulinda maslahi ya wateja wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta utulivu katika sekta ya fedha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amewahakikishia wateja wa Benki ya China kupata huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa hivyo amewatka kuondokana na wasisi wa kukosa stahiki zao zozote kwakuwa mali na fedha zao zipo katika mikono salama.
Benki ya Biashara ya China iliyo na tawi moja Jijini Dar es Salaam, ilipewa leseni na kuanza kufanya shughuli za kibenki hapa nchini mwaka 2015 na kuwa miongoni mwa benki zenye ukuaji wa chini uliosababisha hasara kwenye biashara kwa kipindi chote toka kuanza kwake, na hadi kuchukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania, benki hiyo ilikuwa na mali zisizozidi Shilingi Bilioni 5.
Aidha, Sheria ya mabenki na Taasisi za fedha ya mwaka 2006, imeipa Benki Kuu ya Tanzania Mamlaka ya kusimamia shughuli zote za benki na Taasisi za fedha nchini kwa lengo la kuhakikisha uimara naa uhimilivu wa sekta ya kibenki na fedha kwa ujumla.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato