January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya Tumbaku yajivunia mchango wake sekta ya kilimo

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavii.

BODI ya Tumbaku Tanzania imemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukuza sekta ya kilimo hapa nchini kwa usimamizi wa kipekee ulioleta mageuzi makubwa kwenye zao hilo la biashara.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Stanley Mnozya ametoa shukrani hizo wakati akizungumza na Timesmajira katika mkoa wa Katavi baada ya kukamilika kwa ziara ya kikazi ya siku nne ya Rais Dkt.Samia.

Mnozya amefafanua kuwa miaka mitatu iliyopita uzalishaji ulikuwa kilogram Milioni 37 kwa msimu uliopita waliweza kuzalisha tumbaku kilogram Milioni 123 na kwa msimu huu bado masoko yaendelea na zaidi ya kilogram 111 zimenunuliwa.

Amesema serikali inafanya kazi kubwa ya kutengeneza mazingira mazuri ya kibiashara kwenye sekta ya tumbaku kwani kwa sasa imepanda na yote hayo yamefanywa na Rais Dkt.Samia kwa kuwatendea haki wakulima kufaidika.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa msimu uliopita kulikuwa na shida ya dola duniani na kuna baadhi ya nchi zilihangaika kufanyia malipo kwa wakulima kwa wakati lakini Rais Dkt.Samia kupitia waziri wa Kilimo uliwekwa utaratibu mzuri ili kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati.

“Waziri wa kilimo Hussein Bashe amekuwa akifanya kazi kubwa usiku na mchana kwa kuisimamia vizuri Sekta ya Tumbaku na kwa hayo mabadiliko huwezi kuacha kumsema mchango wake mkubwa aliutowa,”amesema Mnozya.

Amefafanua kuwa maboresho makubwa katika sekta ya Kilimo hususani kwa upande wa zao la tumbaku umefanywa na serikali kwa sababu zao hilo lina mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi kwa Taifa.

Mkoa wa Katavi kwa msimu wa mwaka huu uzalishaji umeongezeka kutoka kilogram Milioni 6 za msimu uliopita na kufikia kilogram Milioni 11 ambapo tayari makampuni ya melipa fedha dola 25,000,000 ambazo ni sawa na Bilioni 67.

“Malipo hayo ya fedha ifahamike kuwa katika ngazi ya halmashari pekee zimenufaika kwa kupata mapato ya fedha zaidi ya Bilioni 2 kutoka mauzo ya zao la tumbaku kwa msimu huu haya nimapinduzi makubwa” Amesisitiza Mkurugenzi huyo.

Emanuel Kachele, Mwanachama wa Amcos ya Filimule Wilaya ya Mpanda amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa kazi nzuri kwani zao la tumbaku hapo awali lilikuwa ni tatizoa ambalo wakulima walishindwa kunufaika nalo.

Mkulima huyo amesema baada ya makampuni ya ununuzi wa zao la tumbaku kuongeza ushindani umekuwa mkubwa kwa makampuni hayo ambapo umezaa matokeo ya wakulima kunufaika.

Agripina Cosmas, Mkulima wa zao la tumbaku amesema toka ameanza kilimo cha tumbaku alikuwa haja wahi kupata malipo kwa haraka kama msimu huu kwani wameweza kulipwa ndani ya mwezi mmoja toka wauze tumbaku yao.

Amesema kazi kubwa imefanywa na Rais Dkt.Samia na Waziri wa kilimo Bashe kwa kuweza kuwajali wakulima wa tumbaku hadi wadogo na hivyo wao hawatawaangusha katika uzalishaji .