Na Jackline Martin, TimesMajira Online
MADEREVA bodaboda na bajaj wametakiwa kuvaa sare za eneo lao husika pale wanapokuwa barabarani na watakaokiuka agizo hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Hatua hizo za kisheria ni pamoja na kutozwa faini ya sh. 25,000 ambayo watatakiwa kuilipa hapo hapo na wakienda kuilipia Mahakamani watalipa sh. 50,000 na anaweza akanyang’anywa leseni ya usafirishaji inapotokea kwamba anafanya makosa ya kukiuka kanuni hizo.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Leseni Mwandamizi wa Mamlaka ya Udhibiti usafiri Ardhini – LATRA, Ngereza Pateli, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa sare za waendesha bodaboda utakaofanyika Juni 29, mwaka huu katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Alisema kwa mujibu wa kifungu Cha 16 (D) ya kanuni za leseni za usafirishaji kwa vyombo vya kukodiwa ikiwemo bodaboda pamoja na bajaji inaelekeza kwamba mwenye pikipiki au bajaji ni sharti dereva wake sare ambayo imekubalika na Mamlaka pamoja na mashirikisho yao.
“Uvaaji wa sare inaangukia kwenye kanuni za leseni ya usafirishaji, vyombo vya kukodiwa ikiwemo bodaboda na bajaji ni sharti kwamba kila mmoja anayetoa huduma hiyo ya usafirishaji ahakikishe amevaa, mfano kwenye upande wa daladala tulikubaliana kwamba sare ya Mkoa wa Dar es Salaam ni ya aina fulani, ni hiyo hiyo itavaliwa na kila mmoja,” alisema.
Alisema mbali na kuzindua sare hizo, aliwasihi waendesha bodaboda na bajaji kuhakikisha na Leseni ya usafirishaji ambapo sharti namba moja ni kuvaa sare hizo.
Aliwakaribisha waendesha bodaboda na bajaj wote kwenye uzinduzi wa sare hizo ili pia waweze kurasimisha biashara yao na huduma yao ipendwe na kila mtu.
Kwa upande wake Meneja wa maendeleo ya Biashara-CRDB Bank Foundation, Happy Mwalusamba, alisema kupitia programu yao ya IMBEJU, katika ushirikiano huo wamejipanga kikamilifu kutoa elimu ya fedha kwa madereva wa Bodaboda pamoja na kutoa mitaji wezeshi ya Shilingi 236,000 kwa kila dereva.
Alisema mitaji hiyo itasaidia katika kupata sare maalum ikiwa ni sehemu ya utambulisho wao, pamoja na ada ya usajili na michango ya kuanzia ya Chama kwa kipindi cha mwaka mmoja pindi Saccos itakapomaliza usajili.
Pia alisema kupitia ushirikiano huo, madereva hao wataweza kuunganishwa na
akaunti ya IMBEJU isiyo na makato. “Akaunti hii itawawezesha kupokea malipo kwa urahisi, kupata bima ya biashara pamoja na fursa nyingine nyingi ikiwemo mafunzo na mtaji wezeshi,” Alisema
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Kagomba, alisema uzinduzi huo ya sare utahusisha madereva bodaboda na Bajaji wa Wilaya ya Temeke, Kigamboni, Ubungo, Kinondoni na Ilala.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria