March 28, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Biteko asikitishwa upotevu wa maji,atoa maelekezo,Muwsa yabeba tuzo mbili za EWURA

Na Martha Fatael, TimesMajira online

NAIBU waziri mkuu na waziri wa Nishati, Doto Biteko ameelezea kusikitishwa kwake na upotevu wa zaidi ya Sh Bil 114.12 zinazochangiwa na uchakavu wa Miundombinu na wizi wa maji katika mamlaka za maji nchini.

Biteko amesema hayo wakati wa uzinduzi wa taarifa ya utendaji wa mamlaka za maji kwa mwaka wa fedha 2023/24 iliyoandaliwa na mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji nchini (Ewura).

Amesema fedha hizo zingetosha kuanzisha mradi mpya na mkubwa wa maji ambao ungejibu changamoto za maelfu ya watanzania ambao Bado hawajafikiwa na huduma hiyo nchini.

Upotevu huo umo katika taarifa ya Ewura kwamba upotevu wa maji katika mamlaka za maji nchini ni asilimia 36.

Kutokana na Hali hiyo, Biteko imetaka Ewura, kwa kushirikiana na mamlaka za maji nchini, kudhiti upotevu huo katika kipindi kifupi kijacho.

Ametaka Ewura, Mamlaka za maji na wadau wengine kuweka mipango madhubuti katika kudhibiti upotevu unaotajwa lakini pia kujihusisha na usafi wa mazingira.

Ametaka mamlaka kuhakikisha zinatekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025 iliyotaka Upatikanaji wa maji kwa vijijini kufikia asilimia 85 nasilimia 95 maeneo ya mijini Ifikapo 2025.

Amesema kwa taarifa aliyopewa Hadi sasa watu wa mjini waliounganishwa na maji ni asilimia 84 ha vijijini ni asilimia 79.6.

Katika uzinduzi huo, Ewura, imetoa tuzo mbili kwa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira mjini Moshi (MUWSA), kati ya mamlaka 19 zenye wateja zaidi ya 20,000 nchini.

Tuzo hizo ni mamlaka Bora ya utoaji wa huduma ya Maji safi na usafi wa mazingira pamoja na ile ya kufikia kwa ufanisi malengo iliyojiwekea katika mipango ya biashara.

Kwa Mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkurugenzi mkuu wa Ewura, Dkt James Andilile, amesema jumla ya vigezo sita vilitumika kupata washindi.

Ametaja vigezo hivyo kuwa ni Upatikanaji wa huduma ya Maji safi,ubora wa maji, jinsi ya kudhibiti upotevu wa maji, uendelevu wa utoaji wa huduma ya Maji, usimamizi wa fedha na jinsi ya kuridhisha wateja.

Amesema kabla ya kupata mshindi Ewura inapokeaa taarifa katika mamlaka husika kisha baadaye huzihakiki.

Amesema mamlaka ziligawanywa katika makundi matatu, Moja zenye wateja wasiozidi 5000, zenye wateja kuanzia 5000 Hadi 20,000 na tatu ni zenye wateja zaidi ya 20,000.

Aidha Naibu waziri mkuu ametaja mamlaka Tano zenye upotevu mdogo wa maji ambazo ni Maganzo wenye upotevu wa asilimia 4, Nzega asilimia 6,Ashuasa asilimia 11,Biharanuro asilimia 12 na Mwanuzi asilimia 13.

Hata hivyo waziri ametaja mamlaka zinazofanya vibaya katika upotevu wa maji nchini ni Rombo yenye asilimia 70, Handeni asilimia 69, Mugambo kyabakali asilimia 64, Ifakara asilimia 56 na Kilindoni asilimia 55.

Awali Mwenyekiti wa bodi ya Ewura, Prof Mark Mwandosya ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwaeleza katika sekta ya maji.

Ametoa mfano mwaka 2011/2012 aliyekuwa waziri wa maji katika bajeti yake amesema maendeleo ya sekta ya maji ilitengewa Sh Bil 206 ambapo mwaka huu wa 2024/25 sekta hiyo imetengewa Sh Bil 558.

Mapema,waziri wa maji Juma Aweso, amesema awali sekta hiyo miaka ya 2018 alikutana na changamoto kadhaa ikiwamo usomaji wa Mita usiozingatia taratibu.

“Mwaka huo nikiwa nyumbani,walikuja wasoma Mita na kutaka kukata maji… nikataka msomaji aniambie amesoma Nini kwenye Mita lakini ukweli halisi hata zile namba za mita hazisomeki vizuri” amesema.

Amesema pamoja na kuwatambua wakurugenzi waliofanya vizuri lakini pia alitaka wanaofanya vibaya watambuliwe ili kuweza kuchukua hatua.

Aweso ametaka mamlaka kuthaminisha viwango vya upotevu wa maji kwa asilimia katika thamani ya fedha ili kuona ukubwa wa tatizo linalooatokana Kila mwezi ama mwaka.