December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Biteko aagiza vyama vya ushirika kujisajili Bima ya mazao

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

VIONGOZI wa Vyama vya Ushirika nchini wametakiwa kuhakikisha vyama vyao vinasajiliwa kwenye mfumo wa Bima ya Mazao ili kuwezesha wakulima wanaopata hasara ya mavuno kutokana na ukame au mvua nyingi kulipwa fidia.

Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini Dotto Mashaka Biteko alipokuwa akihitikisha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Tabora.

Amesema kuwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo majanga ya mvua na upepo mkali ni muhimu sana kwa vyama vya ushirika kuwa na bima ya mazao ambayo itawezesha wakulima kulipwa f idia ya mazao yao.

Amebainisha kuwa kuanzishwa kwa Bima ya Mazao ni mkakati maalumu wa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa kumsaidia mkulima inapotokea majanga ya aina yoyote na kuathiri mazao yao.

Aidha Biteko amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ikiwemo kuzindua utoaji bima za mazao kwa vyama vya ushirika ili kumnusuru mkulima na madhara ya hali ya hewa.

Aidha Naibu Waziri Mkuu ameelekeza makampuni yote yanayonunua mazao ya wakulima kuhakikisha yanarejesha sehemu ya faida wanayopata kwa kuchangia maendeleo ya wananchi katika eneo husika.

‘Nashukuru baadhi ya makampuni yameanza kutekeleza hili katika maeneo mbalimbali, naomba makampuni yote tuige mfano huu, Wizara ya Kilimo wekeeni utaratibu vizuri ila kila kampuni ihusike’, amesema.

Ili kilimo kiendelea kuleta tija kubwa kwa wananchi hasa wa vijijini amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha Maafisa Ushirika wanakuwa na program za kusaidia wakulima vijijini ikiwemo kusikiliza kero zao na kizatatua.

Aidha Biteko amewaomba wanahabari kuendelea kuutangaza ushirika hapa nchini kupitia vyombo vyao ili ufahamike kwa wananchi wote, pia alidokeza kuwa serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa nane nane Ipuli.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewahakikishia wakulima kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuinua sekta ya kilimo kwa kiasi kikubwa na hivi karibuni alielekeza kuanza kutolewa bima ya mazao kwa wakulima wote.

Aidha ameongeza kuwa kwa msimu ujao wa kilimo serikali imetenga sh bil 300 kwa ajili ya kugharamia mbolea ya ruzuku kwa wakulima pia imetenga sh bil 21.4 za kuendeleza ushirika nchini huku Wizara hiyo ikitengewa bajeti nono ya tril 1.23.