Na Jonas Kamaleki, TimesMajira online
SERIKALI itatumia takribani Shilingi bilioni 520 kuwapatia maji safi na salama wakazi wa Mkoa wa Arusha na maeneo jirani na hivyo kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji eneo hilo.
Akizungumza na maafisa wa Idara ya Habari (MAELEZO) hivi karibuni,Mratibu wa Mradi huo, Mhandisi Gasto Francis Mkawe anasema Serikali imeazimia kuboresha miundombinu ya maji jijini Arusha na maeneo ya jirani.
Serikali imewekeza katika kuboresha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira katika Jiji la Arusha ili kuondoa kero ya upungufu wa maji safi na uondoaji wa majitaka katika Jiji la Arusha na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Arumeru ili kuendana na kasi ya ukuaji wa jiji hilo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mkawe,anasema kuwa mradi utaongeza uzalishaji wa maji toka wastani wa lita 40,000,000 hadi lita 200,000,000 kwa siku. Uhitaji wa Jiji la Arusha kwa sasa ni lita 106,000,000 kwa siku, kukamilika kwa mradi huu kutawezesha utoaji wa huduma ya maji kwa zaidi ya asilimia 100.
Licha upatikanaji wa maji safi na salama utakaotokana na mradi huo, zaidi ya Watanzania 2,000 wameajiriwa. Mradi huo umewanufaisha wananchi, takriban sh. bilioni 3 ikiwa ni fidia kwa kutwaa maeneo yao kwa ajili ya ujenzi miundombinu ya mradi huo.
Mradi huo utahusika pia kuboresha huduma za usambazaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka kwa kuongeza mtandao wa bomba za maji kutoka asilimia 44 hadi asilimia 100 ambapo jumla ya takribani kilometa 600 za mabomba za maji zitajengwa.
Sanjari na hilo,jumla ya matanki 11 ya kuhifadhia maji yenye ujazo mbalimbali kuanzia lita 1,000,000 hadi lita milioni 10 na kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji wa jumla ya lita 45,500,000 yatajengwa.
Hili litaenda sambamba na kuongeza mtandao wa kukusanya majitaka kutoka asilimia 8 hadi asilimia 30 kwa kujenga kilometa 192 na kukarabati kilometa 15 za mtandao wa maji taka.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mkawe,yatajengwa mabwawa 18 mapya ya kutibu majitaka yenye uwezo wa kutibu lita milioni 22 kwa siku.
“Mradi huu utaongeza idadi ya wakazi wanaopata maji safi kutoka wastani wa watu 325,000 hadi kufikia watu 600,000 wakiwemo wastani wa watu 250,000 wanaoingia na kutoka jijini Arusha kila siku na wakazi wapatao takribani 159,348 kutoka katika Wilaya za Arumeru, Hai mkoani Kilimanjaro na Simanjiro mkoani Manyara ambao watapitiwa na miundombinu ya mradi, na hii itafanya jumla ya wanufaika wa mradi kufikia zaidi ya milioni moja (1,009,348).
“Kuongeza mtandao wa kukusanya majitaka kutaongeza idadi ya wananchi wanaotarajiwa kupata huduma ya uondoaji majitaka kutoka wastani wa watu 30,000 wa sasa hadi kufikia watu 201,811 mradi huu utakapokamilika” anaongeza Mratibu wa Mradi, Mhandisi Mkawe.
Mradi huo unazo faida nyingine kama vile kuongeza ajira kwa wananchi, kuongezeka kwa masoko kwa viwanda vya ndani vinavozalisha vifaa vya ujenzi kama mabomba,saruji na nondo, fidia kwa wanaopitiwa na mradi na kujengwa kwa miundombinu mingine kama umeme, barabara katika baadhi ya maeneo ambapo miundombinu ya mradi inajengwa.
Mhandisi Mkawe anabainisha kuwa utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 60 ambapo matokeo yake yameanza kuonekana kwa baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa uchimbaji wa visima 11 katika eneo la Magereza Seed Farm, ambavyo vina uwezo wa kuzalisha jumla ya lita milioni 24 kwa siku.
Aidha,visima vingine saba vimeanza kuzalisha jumla ya lita zaidi ya milioni 19 kwa siku na kufanya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) kuwa na uzalishaji lita milioni 64 kwa siku. Ongezeko hili limewezesha AUWSA kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 37.8 na kufikia asilimia 60.
Uchimbaji wa visima virefu 30 katika eneo la Valeska-Mbuguni na Majimoto umekamilika na kutoa matokea mazuri kwa kupata maji mengi zaidi ya matazamio.
Hatua nyingine iliyofikiwa na mradi huu ni kukamilika kwa ujenzi wa mabwawa18 ya kutibu maji yenye uwezo wa kusafisha lita milioni 22 za majitaka kwa siku.
Ujenzi wa bomba za kukusanya majitaka zenye urefu wa takribani kilometa 130 umekamilika kati ya kilometa 200 zilipangwa kufanyika na wateja wapya 1,700 wameungwa.
Bomba kubwa linalopeleka majitaka kwenye mabwawa mapya kutokea eneo la zamani lenye urefu wa takribani kilometa 16 limekamilika na sasa majitaka kutoka eneo la katikati ya mji yameanza kuingia katika mabwawa mapya.
“Tumejipanga sisi AUWSA kutekeleza miradi ya majisafi kwa ufanisi na kwa wakati ili kuhakikisha wananchi katika maeneo haya wanapata huduma ya majisafi na salama kwa wakati,AUWSA itaendelea kutekeleza miradi inayoendelea kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ya kuwapatia wananchi majisafi na salama yenye kutosheleza mahitaji”, anasisitiza Mhandisi Gasto Francis Mkawe.
“Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha dhamira ya dhati ya kuondoa kero ya maji katika jamii, au kama inavyojulikana kama kumtua mama ndoo kichwani.
Katika kutekeleza azma hiyo ya Serikali imetumia sh.trilioni 1.916 kutekeleza miradi 1,845 ya maji na kuwanufaisha wananchi wapatao 14,726,600,” anasema aliyekuwa Msemejaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi jijini Dodoma hivi karibuni.
Akizungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari hivi karibuni jijini Dodoma,Dkt.Abbasi anasema lengo la Serikali ni kuhakikisha inamaliza kero za maji zilizosalia kwenye maeneo machache nchini.
“Hadi Februari 2021, Serikali imetekeleza jumla ya miradi 1,845 yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.916 na kunufaisha wananchi wapatao 14,726,600. Kati ya miradi hiyo, 222 ni ya mijini na miradi 1,623 ni ya vijijini”, amesema Dkt. Abbasi.
“Maji hakuna ‘compromise’ jua litokee au kukuche na giza tunataka maji, asiliamia 95 mijini na asilimia 85 vijijini mpaka mwaka 2025.
“Mtakwenda kufanya nini mtajua wenyewe mimi nataka kama Ilani ilivyoagiza maji yapatikane. Najua mna miradi mikubwa, mna mradi wa kutoa maji Victoria kule kuyaleta mpaka Singida na Dodoma kama ni ndoto kama ni mradi wa kweli nataka utimie.
“Nione maji yamefika Dodoma lakini pia najua kuna mradi wa upande wa Rufiji na wenyewe kama ni stori kwenye makaratasi mimi ninachotaka stori ziwe za kweli.
“Pamoja na miradi mingine midogo midogo ambayo inapeleka maji kwa watu, kinachotakiwa hapa ni asilimia 95 na 85 ifikapo 2025. Tuna deni kubwa sana la wananchi kwenye maji”, anasema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Azma ya Rais Samia ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2025.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia