Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar
SERIKALI kupitia Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo, imesaini mkabata wa ujenzi wa Uwanja wa Dokta Samia Suluhu Hassani wenyewe thamani ya Sh. bilioni 286.
Uwanja huo utatumika katika michuano ya mataifa Afrika AFCON 2027, inayoandaliwa na nchi za Tanzania, Kenya na Uganda
Mbali na hivyo pia, uwanja huo wa mpira wa miguu utajengwa mkoani Arusha, utakaojengwa na Kampuni ya CRJE kutoka nchini China.
Akizungumzia hilo wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa uwanja huo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema uwanja huo utaingiza watu 30,000.
Hata hivyo amesema uwanja huo utakuwa wa kisasa zaidi katika Afrika Masharika kutokana na kusheheni huduma mbalimbali.
Dkt. Ndumbaro amesema, Serikali itahakikisha ujenzi huo unafanywa kwa haraka kwa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) ifikapo mwaka 2027, ikiwa ni juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Amesema, uwanja huo utachagiza kwa kiasi kikubwa utalii wa nchi yetu kwani zitafanyika shughuli mbalimbali tofauti na mpira wa miguu kama vile mchezo wa riadha, pamoja na biashara zitakazokuwa zinafanyika uwanjani hapo.
“Uwanja huo utakuwa na ubora wa hali ya juu kwani utakuwa na vyumba vya watu mashuhuri pande zote mbili za uwanja zoezi hili limefanyika leo (jana) ambapo, Rais Samia akiwa anatimiza miaka mitatu ya uongozi wake,” alisema Ndumbaro.
Aidha, aliipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya elimu Utamaduni na Michezo kwa juhudi iliyofanya mpaka kukamilisha zoezi hilo ambalo limechukua muda mrefu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, amewataka wakandarasi wa uwanja huo wahakikishe ujenzi unakamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
“Wakandarasi hakikisheni kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025, uwanja uwe umefikia kiwango kinachoridhisha na utekelezaji huo uanze haraka iwezekanavyo ikiwa ni maandalizi kuelekea katika michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON),”amesema.
Amesema, Kamati itatoa ushirikiano kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kama ilivyokusudiwa na kudai kuwa, Rais Samia anaitendea haki sekta ya michezo kama anavyofanya kwenye sekta nyingine, na kuwataka watu wa Arusha watunze rasilimali za uwanja huo.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, amesema uwanja huo utaongeza idadi ya watalii katika mkoa huo.
More Stories
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi