Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mara
JUMLA ya Sh. bilioni 2.1 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa miradi ya maji ya bomba kutoka ziwa Victoria kwenda vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, katika bajeti ya mwaka 2021/2022.
Hayo yamesemwa jana na Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) wa wilaya hiyo Edward Silonga alipokuwa akizungumzia maendeleo ya uboreshaji wa huduma ya maji wilayani.
Serikali imetenga Sh. bilioni 2.1 katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji kwenye baadhi ya vijiji vikiwamo vya Mikuyu Chumwi, Mabuimerafuru, Seka na Kaboni,” amesema Silonga.
Meneja huyo amevitaja vijiji vingine kuwa ni Bugoji, Kaburabura, Kanderemba, Kiriba Bwai Kumsoma na Bwai Kwitururu, Bugwema Masinono, Muhoji, Kinyang’erere na Murangi na Lyasembe.
“Vijiji vingine ambavyo vitafikiwa na mradi huo wa maji ili kupunguza kero ya ukosefu wa huduma hiyo ni Mwiringo, Maneke, Kwikuba, Nyegina Nyegina, Mkirira na Kurukerege,” amesema.
Amefafanua kuwa wilaya hiyo ina vijiji 68 na kata 21, ambapo kila kata imetengewa fungu fedha kwa ajili ya mradi wa maji, huku akitolea mfano Kata ya Bugoji kuwa imetengewa Sh. milioni 227.9.
“Katika kata hii kuna vijiji vitatu vya Bugoji, Kaburabura na Kanderema, na itakuwa na vituo 16 vya kupokea maji kutoka ziwa Victoria na wanufaika wa maji hayo ni watu 10, 328,” amesema.
Amesema. mbali na miradi hiyo, ipo mingine ya nyuma ya bajeti ya mwaka 2020/2021 ambayo imekamilika na kuzinduliwa, ambapo sasa wananchi wanaendelea kupata huduma hiyo muhimu.
“Bejeti ya 2020/2021 ilikuwa ni Sh. bilioni 1.3, imesaidia kukamilisha baadhi ya miradi, kwa mfano Kijiji cha Bukima, tayari wananchi wanapata huduma hiyo, tunaendelea kukamilisha mingine zaidi,” amesema.
Aliitaja miradi mingine ya maji inayokamilishwa kuwa ni vijiji vya Suguti na Kusenyi unaogharimu Sh. milioni 84 na mwingine kutoka Suguti hadi vijiji vya Kwikonero, Rwanga na Kasoma wenye thamani ya Sh. milioni 80.
“Lakini pia kuna mradi wa maji wa vijiji vya Butata na Kastamu ambao gharama yake ni Sh. milioni 286.1, jumla ya gharama za miradi hiyo yote ni Sh. milioni 450.1,”amesema.
Amesema, RUWASA inaendelea kutandaza miundombinu zikiwamo pampu za za kusukuma maji kwenda vituo mbalimbali vya vijiji ambavyo viko mbali na ziwa Victoria ili viweze kupata huduma hiyo.
Kuna vijiji ambavyo viko umbali wa zaidi ya kilomita 15 kutoka ziwa Victoria, na vinatakiwa kupata maji, hivyo RUWASA inajenga miundombinu ya kuwezesha kila kijiji kupata maji,” amesema.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi