Na Allan Kitwe, Tabora
HALMASHAURI ya manispaa Tabora imemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea zaidi ya sh bil 51 tangu aingie madarakani mwaka 2021 hadi sasa kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
Akiongea katika kikao cha robo ya pili ya baraza la madiwani wa halmashauri hiyo jana, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Kapela ameeleza kuwa fedha hizo zimeleta mageuzi makubwa ya kimaendeleo katika manispaa hiyo.
Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo zaidi ya sh bil 7.3 zimetumika kutekeleza miradi ya afya, sh bil 9.4 miradi ya elimu kwa shule za msingi na sh bil 23 kwa shule za sekondari ambapo shule mpya za sekondari zimejengwa katika kata zote.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1001662430-1024x768.jpg)
Aidha kiasi cha sh bil 5 zimetumika kwenye shughuli za utawala huku zaidi ya sh bil 2.5 zikitumika kwenye shughuli za kilimo ikiwemo serikali kutoa ruzuku ya mbolea na mbegu kwa wakulima ili kuboresha shughuli zao.
Mstahiki Meya ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 4 ya uongozi wa Rais Samia wamepokea zaidi ya sh bil 3.8 kwa ajili ya uhawilishaji kaya maskini hali iliyopelekea vijana, akinamama na watu wenye ulemavu kuinuliwa kiuchumi.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 4, serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefikisha huduma ya umeme katika vijiji 12,301 kati ya vijiji 12,318, vimebakia vijijij17 ambapo utekelezaji unaendelea.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1001662424-1024x768.jpg)
Kwa upande wa Vitongoji, Kapela amesema kuwa hadi sasa zaidi ya asilimia 60 ya Vitongoji vyote vimeshafikishiwa huduma hiyo na wananchi wameendelea kunufaika kwa kuanzisha miradi ya kiuchumi.
Diwani wa Kata ya Gongoni katika manispaa hiyo Kessy Sharif Abdulrahman ameunga mkono tamko hilo na kuitaka halmashauri kusimamia ipasavyo miradi yote iliyoanza kutekelezwa ili ikamilike haraka na kwa wakati kwa manufaa ya wananchi.
‘Serikali ya awamu ya 6 imefanya kazi nzuri sana katika halmashauri yetu, naomba miradi ambayo haijakamilika isimamiwe ipasavyo ili ikamilike kwa wakati, hususani ujenzi wa matundu ya vyoo katika baadhi ya shule’, ameeleza.
Naibu Meya Mstaafu wa Manispaa hiyo Rose Kilimba (diwani wa Kata ya Ifucha) ameomba wakazi wa Mitaa ya Tuli, Usuhilo na Miziwaziwa katika kata hiyo kupimiwa maeneo yao na kumilikishwa ili waishi kwa amani pasipo bughudha.
More Stories
Serikali ipo kwenye maandalizi ya TASAF III,ambao hawajainuka kiuchumi TASAF II kupewa kipaumbele
DC Kilindi ataka jitihada ziongezwe makusanyo mapato ya ndani
Bil.51 zachochea kasi ya maendeleo Manispaa Tabora