January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bil 35 kumaliza kero ya maji Kasulu

Na Allan Vicent, TimesMajira Online

KERO ya maji katika halmashauri ya Mji Kasulu imepata mwarobaini baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kupeleka zaidi ya sh bil 35 ili kuboreshwa miundombinu ya vyanzo vya maji vilivyopo na ujenzi wa tenki kubwa zaidi.

Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kasulu (KUWSA) Mhandisi Athuman Kilundumya alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake.

Amesema wilaya hiyo yenye wakazi zaidi ya 235, 000 ni moja ya wilaya za kimkakati na kibiashara katika Mkoa wa Kigoma ambayo imekuwa na shida kubwa ya upatikanaji maji safi na salama.

Amebainisha kuwa hali ya upatikanaji majisafi katika Mji wa Kasulu ni chini ya asilimia 60, ili kumaliza kero hiyo serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeleta zaidi ya sh bil 35 ili kutekeleza miradi ya kimkakati.

‘Tumepokea zaidi ya bil 35 kupitia mradi wa serikali wa Miji 28 ili kuboresha huduma ya maji katika Mji wetu wa Kasulu, mradi huu utamaliza kabisa kero iliyopo sasa,’ amesema.

Mhandisi Kilundumya amefafanua shughuli zitakazofanyika kupitia fedha hizo kuwa ni ujenzi wa chujio la kutibu maji litakalozalisha maji yenye mita za ujazo milioni 15.

Nyingine ni ujenzi wa matenki 2 Mtaa wa Kumnyika na Rusunwe yenye uwezo wa kuhifadhi lita mil 2.5 za maji na ujenzi wa chanzo kipya kitakachozalisha lita mil 16 kwa siku.

Shughuli nyingine ni ujenzi wa mtandao wa maji wenye urefu wa km 20 ambao utasambaza maji katika maeneo mbalimbali kutoka kwenye tanki kuu.

Kilundumya amesisitiza kuwa Wataalamu wa KUWSA wamejipanga vizuri ili kuhakikisha ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Malpinduzi inatekelezwa kwa vitendo na kuhakikisha wakazi wa Mji wa Kasulu na vijiji jirani wanapata maji safi na salama kwa asilimia 95 kabla ya mwaka 2025.

Naye Afisa wa Mamlaka hiyo Mhandisi Goodluck Shefatia ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umeanza mwezi wa nne mwaka huu chini ya Mkandarasi Mega Enginering Construction Company Ltd na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2025.

Amebainisha mkakati mkubwa wa Mamlaka hiyo kuwa ni kuongeza uzalishaji wa maji, kudhibiti upotevu na kupanua mtandao wa maji katika Mji huo.