November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya TCB yatoa mikopo ya Bil. 700/- kwa wastaafu

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imeendelea kutoa mikopo kwa wastaafu, ambapo hadi sasa imetoa takribani sh. Bilioni 700 kwa ajili ya kundi hilo.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB, Adam Mihayo, wakati akizungumza na waandishi na wahariri wa vyombo vya habari nchini katika kikao kazi kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, kilichofanyika leo Jijini Dar es salaam.

Alisema lengo la kuanzisha mikopo kwa
wastaafu ni kuwawezesha kupata mikopo kwa urahisi, kwani wanapomaliza muda wao kazini taasisi nyingi za fedha zinawasaha kuwakopesha.

“Mpaka sasa tumetoaa takribani sh. Bilioni
700 kwa ajili ya kundi hili maalum ambalo
limetumikia nchi,”alisema.

Aidha, Mihayo alisema wamefanikiwa
kuongeza mapato kutoka sh. Bilioni 43. 7
kwenda sh. Bilioni 56.8, ambapo ongezeko hilo limesababishwa na mapato ya ndani.

“Tunawashukuru wateja wetu kwani wametuwezesha sasa mtaji wetu kukua na tuweze kutoa huduma nzuri zaidi,” alisema.

Mihayo alieleza kuwa kwenye upande wa
huduma za kidijitali, wamefanya mwingiliano na mifumo mbalimbali ikiwemo TRA, GPG,
EMS ili kuwawezesha wateja kufanya miamala mbalimbali na Serikali na taasisi za kiserikali.

“Tunafanya utaratibu wa kulipa mishahara kwa wafanyakazi,kama Kampuni inataka kupitisha mishahara kwetu hiyo huduma tunayo pia kupitia huduma hiyo tunaweza kutoa mikopo kwa wafanyakazi,” alisema Mihayo

Pia alisema, “Tukifanya uwekezaji kwenye
maeneo ya kidigitaji mauzo yataongezeka na kutoendelea kutegemea mapato kutoka kwenye riba na badala yake tuweze kukuza mapato yanayotokana na commercial feez na kushusha gharama za kutoa huduma.”

Aidha, alisema wamekua wakikua mwaka hadi mwaka ambapo mwaka jana amana zimekua kwa takribani asilimia 11, hivyo aliwashukuru wateja wao kwa kuendelea kutuamini.

Pia alisema mikopo imekua ikikua mwaka hadi mwaka, ambapo mwaka jana wamefunga na sh. Bilioni 916 sawa na ukuaji wa asilimia 9 na mwaka huu, mpango mkakati wao ni kukuza zaidi sekta ya wafanyabiashara ambapo wametenga takribani sh. Bilioni 300 kwa ajili ya kuwaunga mkono wafanyabiashara hao.

“Wafanyabiashara wanachangia kwa
takribani asilimia 30 ya ukuaji wa uchumi na tukiunga mkono sekta hiyo ya wafanyabiasharaninamaanisha nafasi zaidi za ajira, lakini pia kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa Serikali”

Kwa upande wa mali, Mihayo alisema hadi
mwaka 2023 wamefunga na sh. trilioni 1.4 na mwaka huu wamejipa changamoto ili wakue mpaka sh. trilioni 1.7.

Kuhusu mtaji, Mihayo alisema kwa mwaka jana walifunga na sh. Bilioni 120 hivyo aliishukuru Serikali kwa kuwaongezea mtaji mwaka 2023 na hiyo imeonesha kwamba Serikali ina imani kubwa na wao na hivyo kuahidi kuendelea kuchapa kazi.

Kwenye upande wa mapato, Mihayo alieleza kuwa yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na taasisi kuaminika na kwa mwaka jana mapato yalikuwa bilioni 184.

Mihayo alisema Katika miaka mitatu ijayo
wanataka wawe benki ya tatu kwa upande wa mali, mikopo na ukwasi.

Kuhusu utoaji huduma bora kwa wateja wao, Mihayo alisema wana makala zaidi ya 6,000 maana yake wapo kila sehemu ya nchi yetu na mwaka huu wanataka wapanuke zaidi kwa kuongeza wakala wengine 4,000 ili waweze kusogeza huduma zaidi kwa wananchi.

Kwa upande Mwingine, TCB inatarajiwa
kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake
nchini.

TCB ni zao la Tanganyika Postal Office
Savings Bank (TPOSB) ambayo ilianzishwa mwaka 1925 wakati ambapo Tanganyika ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza.