January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya TCB yaendelea kuchochea maendeleo ya kiuchumi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imesema inajivunia kuwa sehemu ya mradi wa reli ya kisasa (SGR) uliozinduliwa hivi karibuni kwa safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Akihutubia katika uzinduzi huo jijini Dodoma, Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliuelezea mradi huo kuwa kielelezo cha maendeleo makubwa ya kimiundombinu na ya taifa kwa ujumla na kwamba Kuanza kwa mradi wa SGR ni hatua muhimu katika kutimiza ndoto ya kuwa na miundombinu ya usafiri wa haraka, rahisi na wa kuaminika.

Alifafanua kwamba matokeo ya mradi yanaweza yasionekane mapema, lakini lengo la mradi ni kutoa huduma kwa taifa na mchango wake katika kuwezesha biashara za kimataifa na maendeleo ya nchi na kuwa Sehemu ya mradi huu inayoendelea kujengwa kuelekea Kigoma mpakani mwa nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaonyesha namna mradi huu utakavyonufaisha uchumi wa nchi hasa sekta ya utalii.

Benki ya TCB imepewa heshima kuwa benki mdau namba moja katika mradi huu wa kimageuzi kwa kuwezesha mchakato wa kuagiza vichwa vya treni na mabehewa ya SGR na kutoa mikopo kwa wakandarasi wa Yapi Merkezi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB, Bw. Adam Mihayo amesema Lengo lao ni kuhakikisha kwamba wateja wanafikiwa na kunufaika na huduma za mradi wa SGR kupitia mawakala walioenea nchi nzima na uwezo mkubwa wa programu ya TCB Popote, wanamwezesha kila mmoja kujionea urahisi na uhakika wa usafiri wa kisasa.

Aidha Mihayo ameeleza kuwa Sambamba na hilo , benki ilishinda zabuni ya kutoa huduma za ukusanyaji wa nauli kwa njia za kidijiti ikiwemo kupitia mashine za kukatia tiketi (Ticket Vending Machine) hali kadhalika, programu ya simu ya TCB Popote inayomwezesha mteja kujifungulia akaunti kwa kiasi cha shilingi 1,000 tu, inarahisisha ukataji wa tiketi za SGR mahala popote nchini.

Wateja pia, wanaweza kununua tiketi zao bila usumbufu kwa mawakala 7000 wa Benki ya TCB waliopo nchi nzima, na hivyo kurahisisha upatikanaji wa tiketi na , hivi sasa kadi za ATM zinaweza kutumika katika mifumo ya PoS na mashine za kukatia tiketi (TVM) zilizopo katika stesheni zote.

Mihayo amesema Katika kuwezesha mfumo kufanya kazi kwa ufanisi, Benki ya TCB imezindua mfumo wa malipo wa QR code kwa abiria ili kuwawezesha kutumia mfumo wa PoS bila kuhitaji intaneti kuzuia makosa ya kimfumo.

Aidha, ubunifu wa mfumo wa kimawasiliano unaotumia akili mnemba kupitia mtandao wa WhatsApp unawezesha upatikanaji wa huduma za SGR kwa urahisi na kwamba , makusanyo ya manunuzi ya tiketi yameunganishwa na mfumo wa GePG ili kuendelea kujenga pato la nchi.

Benki ya Biashara Tanzania (TCB) ni taasisi ya kifedha inayoongoza katika utoaji wa usuluhisho wa kifedha unaolenga kukidhi mahitaji wa wateja wake na imekijipambanua katika uchumi jumuishi na maendeleo ya kiteknolojia, Benki ya TCB inajizatiti kuboresha huduma za kibenki na kuchangia katika ukuaji wa uchumi nchini.