November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya Taifa ya ushirika mbioni kuanzishwa

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

TUME ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), imejipanga kuharakisha mchakato wa uanzishwaji wa Benki ya Taifa ya Ushirika ili kuviwezesha Vyama vya Ushirika kupata Mikopo yenye Riba nafuu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo, Agosti 11,2023 kuhusu utekelezaji wa shughuli na mafanikio ya tume hiyo Mrajis wa vyama vya ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt.Benson Ndiege amesema kuwa hadi kufikia Disemba 2024, Tume itakuwa imeshazindua Benki ya Taifa ya Ushirika (KCBL) na kuwa mali ya wanachama katika kujipatia mikopo ya kuendesha shughuli zao kikamilifu.

Pia amesema tume hiyo imejipanga kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya kidijitali ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika Vyama vya Ushirika, pamoja na Mamlaka za Usimamizi.

“Tumejipanga kuhamasisha mfumo wa Ushirika kujiendesha kibiashara wenye kuaminika na shindani ukijikita kwenye kuongeza thamani ya uzalishaji katika Vyama pamoja na kuboresha Sera, Sheria na usimamizi wa Ushirika ili kuchochea ukuaji na maendeleo ya Ushirika imara Tanzania.

Vilevile amesem tume itahamasisha Ushirika kwenye sekta mbalimbali na makundi maalum ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na mfumo wa Ushirika,tuimarisha uwekezaji wa mali za Ushirika katika uzalishaji pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto zilizopo kwenye Ushirika.

Wakati huo huo Mrajis huyo alizingumzia suala la tume hiyo katika Usimamizi na Udhibiti wa Vyama vya Ushirika, ambapo amesema kuwa ilifanya usajili
sajili wa Vyama vya Ushirika na Wanachama mwaka 2022/2023 imesajili jumla ya Vyama vya Ushirika 7,300, kati ya hivyo 77 ni Vyama vya Upili, 1 ni Shirikisho la Vyama vya Ushirika, 4,252 ni Vyama vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS), 2,034 ni Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na 936 ni Vyama vinavyojishughulisha na kazi mbalimbali zikiwemo, ufugaji na uvuvi.

“Tume imeongeza idadi ya wanachama wa Vyama vya Ushirika kutoka wanachama 6,965,272 mwaka 2021/2022 hadi 8,358,326 mwaka 2022/2023,”amesema Ndiege

Aidha amesema kuwa mwaka 2022/2023, tume ilifanya ukaguzi wa jumla ya Vyama vya Ushirika 4,712 na kubaini mapungufu mbalimbali ya kiutendaji, baadae mapungufu hayo yalifanyiwa kazi kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuvunja bodi 55 za Vyama vya Ushirika, kupeleka masuala 30 polisi na masuala 47 yanashughulikiwa na TAKUKURU pamoja na Aidha, kutoa mafunzo kwa watendaji 4,732 wa Vyama vya Ushirika.