December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya Stanbic Tanzania, Agricom kukuza Sekta ya kilimo nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya Stanbic Tanzania (SBT) kwa kushirikiana na kampuni ya zana za kilimo ya AgriCom Africa (AA) zimesaini hati ya makubaliano (MoU) ili kuleta mapinduzi ya kilimo kwa kuongeza matumizi ya zana bora na za kisasa katika kilimo kwa ajili ya kukuza sekta ya kilimo nchini.

Ushirikiano huo utawasaidia wananchi kunufaika na zana mbalimbali za kilimo zilizotengenezwa kwa teknolojia bora na ya kisasa kutoka AgriCom Africa kwa ajili ya kuleta mapinduzi ya kisasa katika sekta ya kilimo na kuongeza uzalishaji.

Akizungumza katika Viwanja vya Nane Mkoani Mbeya, Mkuu wa Kitengo cha Mikopo ya Asseti na Vyombo vya Moto kutoka SBT (Head of Vehicle Asset Financing) , John Mosha amesema kuwa kupitia ushirikiano huo na AgriCom itasaidia wananchi husussani wakulima kuwawezesha kununua zana za kilimo sambamba na kukopa vifaa na mashine mbalimbali za mashambani ili kuongeza ufanisi na uzalishaji wenye tija.

“Ushirikiano huu utakakikisha upatikanaji wa zana za kisasa ambazo ni bora.Wakulima watanufaika na zana hizi za kisasa zitakazoweza kusaidia kuongeza uzalishaji kwenye shughuli za shamba, hivyo kuhamasisha maendeleo ya kilimo biashara kwa kuleta mapinduzi ya kiuendeshaji hali itakayochangia kukuza mafanikio ya sekta ya kilimo biashara nchini.” ameeleza John Mosha.

Aidha, kupitia ushirikiano huo, wananchi pia wataweza kunufaika na mikopo ya kifedha katika sekta ya kilimo biashara kwa zaidi ya silimia 80 kutoka Stanbic Bank huku kukiwa na sharti la muda, ambapo wanaweza kulipa ndani ya miezi 60 (sawasawa na miaka mitano – 5).

Mkuu wa Kitengo cha Biashara kutoka SBT, Fredrick Max ameeleza namna ambavyo benki ya SBT imekuwa ikiwezesha mikopo ya fedha kupitia asseti katika sekta mbalimbali hapa nchini kwa muda mrefu, hivyo imeamua kuja na mpango huu uliojikita katika kukuza mnyororo wa thamani kwenye kilimo biashara kwa kubuni mifumo inayoweza kuongeza uzalishaji, uchakataji na usafirishaji wa mahitaji katika kilimo, ikiwa ni mpango wa kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo biashara na kufikia lengo la mafanikio ya ukuaji wa sekta ya kilimo kwa zaidi ya asilimia 10 kwa mwaka, hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.

“Pamoja na mambo mengine, SBT tumejikita pia katika kulea vijana na wanawake wajasiriamali waliojikita katika kilimo biashara kupitia Programu Biashara Atamizi (Business Incubator program). Programu hii inalenga kuhamasisha vijana na wanawake wajasiriamali walioko katika sekta ya kilimo biashara. Tunawajengea uwezo kwa kuwasaidia kujenga mtandao wa kitaasisi kwenye sekta ya kilimo, pamoja na kuwaunganisha na wadau muhimu kwenye mnyororo wa thamani ndani ya sekta ya kilimo biashara,” ameeleza Max.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni za AgriCom (AgriCom Group), Alex Duffar ameeleza kuwa sekta ya kilimo nchini Tanzania ni muhimu kwakuwa inachangia katika pato la taifa kwa asilimia 65, ambapo makubaliano yaliyosainiwa leo kati ya kampuni yake na SBT yanalenga kuchagiza matumizi ya zana za kilimo ambazo ni bora na za kisasa kwenye kilimo, hivyo kukuza uchumi na maendeleo ya viwanda nchini na kujenga msingi endelevu wa mifumo ya usalama wa chakula katika Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika.

“AgriCom Africa tumejizatiti kuhamasisha matumizi ya zana za kilimo kupitia ushirikiano kama huu ambao leo tumeuingia na Stanbic Bank Tanzania.

Hati ya Makubaliano iliyosainiwa leo itawawezesha wakulima kupata zana bora za kilimo. Ushirikiano huu utasaidia wakulima kukopa fedha za kununulia zana bora za kilimo.”

AgriCom Africa ikiwa ni kampuni inayojulikana kwa ubunifu wake katika zana za kilimo, leo tutawaonyesha pia bidhaa yetu ya hivi karibuni ambayo ni mashine inayotumika baada ya mavuno (Post-harvest management—the Mobile Grain Dryer) na 4WD drivelines kwa ajili ya trekta kama vile Kubota EK4-751.” ameeleza Afisa Mtendaji wa AgriCom Group.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Juma Homera amesema mikoa ya nyanda za juu kusini inaongoza kwa kilimo nchini Tanzania, hivyo makubaliano haya yataongeza thamani ya sekta ya kilimo na kusaidia wakulima kuondokana na kilimo kinachotumia zana duni badala yake watatumia mashine za kisasa katika uzalishaji.

“Kilimo cha sasa ili ufanikiwe unahitaji mashine za kisasa, hivyo makubaliano haya yatawezesha zana za kilimo kwa wakulima kati ya benki ya Stanibic ambao wako karibu Afrika nzima wataweza kurahisisha kilimo hatimae kusaidia adhma ya serikali ya kwamba ifikapo mwaka 2030 Tanzania iongeze uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa asilimia 10″ amesema Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara kutoka SBT, Fredrick Max amesisitiza kuwa ushirikiano huo unalenga kuunga mkono kauli mbiu ya iliyotolewa na Wizara ya Kilimo ya kwamba, ‘Kilimo ni Biashara’ ambapo ushirikiano huo unalenga kukuza uwekezaji wa sekta binafsi kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo ili kufikia malengo ya ukuaji wa sekta ya kilimo asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Mkuu wa Kitengo cha Mikopo ya Asseti na Vyombo vya Moto kutoka SBT (Head of Vehicle & Asset Financing) , John Mosha na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni za AgriCom (AgriCom Group), Alex Duffar, wakitia saini leo kwenye hati ya makubaliano (MOU), ambapo wananchi wataweza kunufaika na zana mbalimbali za kilimo zilizotengenezwa kwa teknolojia bora na ya kisasa kutoka AgriCom Africa kupitia mikopo ya kifedha katika sekta ya kilimo biashara kutoka Stanbic Bank Tanzania (SBT).
Mkuu wa Kitengo cha Mikopo ya Asseti na Vyombo vya Moto kutoka SBT (Head of Vehicle & Asset Financing) , John Mosha na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni za AgriCom (AgriCom Group), Alex Duffar, wakionyesha hati ya makubaliano waliyosaini leo, ambapo wananchi wataweza kunufaika na zana mbalimbali za kilimo zilizotengenezwa kwa teknolojia bora na ya kisasa kutoka AgriCom Africa kupitia mikopo ya kifedha katika sekta ya kilimo biashara kutoka Stanbic Bank Tanzania (SBT).
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Juma Homera ambaye ni mgeni rasmi tukio la utiaji saini wa hati ya makubaliano kati ya Stanbic Bank Tanzania (SBT) na AgriCom Africa (AA) akizindua moja ya zana za kilimo wakati wa tukio hilo lililofanyika leo kwenye maoneyesho ya Nane Nane Jijini Mbeya.
Timu ya wafanyakazi wa Stanbic Bank Tanzania (SBT) na kampuni ya zana za kilimo ya AgriCom Africa (AA) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya tukio la utiaji saini wa hati ya makubaliano kati ya Stanbic Bank Tanzania na AgriCom Africa kwa ajili kuleta mapinduzi ya kilimo kwa kuongeza matumizi ya zana bora na za kisasa katika kilimo kwa ajili ya kukuza sekta ya kilimo nchini.