Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Benki ya NMB imeanzisha mpango maalum wenye masuluhisho mahususi kwaajili ya kuwahudumia Wastaafu na Wastaafu watarajiwa unaoitwa NMB Hekima Plan wenye Kauli Mbiu “Staafu Kifahari”
Akizungumza katika warsha iliyowakutanisha Wastaafu na Wastaafu watarajiwa zaidi ya 400 jijini Dodoma kwa ajili ya kuwaelimisha na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za maisha baada ya ajira, Mkuu wa Idara ya Biashara ya Serikali wa benki hiyo, Bi. Vicky Bishubo alieleza kuwa, masuluhisho yaliyomo kwenye NMB Hekima Plan ni pamoja na mikopo mbalimbali ikiwemo ile ya nyumba, ambapo mkopaji anaweza kupata hadi Tsh. bilioni 1.
Kupitia utaratibu huu, wastaafu watapewa pia elimu ya ustawi wa afya na usalama wa fedha zao huku wakionyeshwa fursa mbalimbali za uwekezaji. Lakini pia, NMB Hekima Plan ina bima za afya na mali za gharama nafuu na bei shindani sokoni.
Zipo pia Akaunti maalumu zisizokuwa na makato ya mwezi ambazo zinampa nafasi mstaafu kupata mkono wa pole wa hadi Tsh milioni 2 endapo yeye au mwenza wake atafariki na kumwezesha kupata kiasi kama hicho akipata ulemavu wa kudumu.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa program hii, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako aliipongeza Benki ya NMB kwa kuja na utaratibu huu ambao lengo lake kubwa ni kusaidia kuenzi mchango mkubwa wa watumishi hawa katika ujenzi wa taifa.
Aliongeza kuwa pia ni suala la thamani na azma ya Serikali kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii na kuhakikisha kuwa Wastaafu si tu wanaishi maisha bora na ya Furaha, lakini pia kuhakikisha wanaendelea kuchangia juhudi za ujenzi wa taifa.
“Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uendeshaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchni, ili wastaafu waweze kuchangamkia fursa zinazoletwa na taasisi za fedha kama huu mpango wa NMB Hekima Plan,” Prof Ndalichako alisema.
Akisisitiza umuhimu wa wastaafu kuwa na nidhamu ya fedha na matumizi ya pensheni zao, Waziri alibainisha kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali kuiimarisha sekta hiyo ni pamoja na kuboresha mifuko ya hifadhi ya jamii na utoaji wa huduma kwa ujumla.
Aidha, alisema uwekezaji unaofanywa kubuni masuluhisho ya kidijitali na Benki ya NMB yatasaidia si tu kuwahudumia wastaafu lakini pia upatikanaji wa huduma kwa watu wote na kuwasihi Wastaafu kuzingatia mafunzo na maarifa watakayopewa na wataalum ili waweze kuzikabili changamoto hizi. Zoezi la kutoa elimu litafanyika kwa Wastaafu litafanyika nchi nzima.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa