January 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NMB yatoa fidia ya shilingi milioni 270 kwa wahanga wa mafuriko Hanang

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya NMB kwa kushirikiana na kampuni ya bima ya Reliance Insurance wamekabidhi hundi ya shilingi milioni 270 zitakazotumika kuwalipa fidia wajasiriamali wadogo na wa kati 18 walioathirika na maporomoko ya matope yaliyotokea wilayani Hanang, mkoani Manayara Desemba 3, 2023 na kuwaacha watu wengi na hasara kubwa.

Hii ni kutokana na wajasiriamali hao kulipa bima ya mikopo ambayo walipata kutoka benki ya NMB kabla kabla ya janga hilo kutokea mwanzoni mwa Disemba mwaka jana.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika Stendi ya Mabasi ya Katesh mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Idara ya Bima ya benki ya NMB, Martin Massawe amesema benki yake inaamini kuwa bima ina nafasi kubwa katika usimamizi wa hatari kwa wafanyabiashara na kuongeza kuwa mpango wa fidia wa benki hiyo unalenga kutoa ahueni ya kifedha kwa wateja 18 wa benki hiyo ambao walikata bima ya mikopo yao awali.

“Wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wanakabiliwa na changamoto nyingi hivyo kukosa uhakika wa shughuli zao. Katika suala hili, bima ni zana muhimu ambayo inaweza kutoa ahueni kwa biashara, kuwalinda kutokana na matukio yasiyotarajiwa ambayo yanaweza kuhatarisha maisha na mafanikio yao, “amesema.

Massawe amebainisha kuwa benki yake imedhamiria kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya bima kuanzia katika ngazi za chini nchini kote kama sehemu ya juhudi za benki hiyo kusaidia ukuaji na biashara za ndani.

“Tumekusanyika leo katika hafla hii adhimu ya kukabidhi fidia ya takriban shilingi milioni 270 kwa wateja wetu 18 walioathiriwa na maporomoko ya matope wilayani Hanang. Kwa bahati nzuri, mikopo waliyopata kutoka benki yetu ilikuwa na bima. Fidia hii itakuwa ni afueni kubwa kwa wananufaika wote na nimatumaini yangu kuwa sasa watakuwa katika nafasi nzuri ya kuendesha biashara zao bila matatizo, Massawe” amesema.

Massawe amewataka wafanyabiashara mkoani Manyara kujiunga na bima mbalimbali zinazotolewa na benki yake ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza.

“Benki yetu inatoa bidhaa mbalimbali za bima zilizoboreshwa na kutengenezwa mahususi kwa watu wote kuanzia ngazi za chini na bei zake ni kuanzia shilingi elfu 10 tu kwa mwaka. Uzuri ni kwamba taratibu za uandikishaji zimerahisishwa kidogo ili kuvutia watu wengi kuanzia katika ngazi za chini,” ameongeza.

Amebainisha kuwa mwaka huu benki hiyo itaanza kampeni maalum ya kuhamaisha matumizi chanya ya bima itakayoenda sambamba na utoaji wa elimu ya bima nchi nzima kama sehemu ya dhamira ya benki hiyo kusaidia ukuaji wa sekta ya bima.

Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware wakati wa hafla hiyo amebainisha kuwa ulipaji wa fidia hiyo ni utekelezaji matakwa, kanuni na taratibu za kisheria huku akishukuru benki ya NMB na kampuni ya bima ya Reliance kwa kutekeleza utaratibu huo ndani ya muda muafaka.

“Bima inahakikisha mtu kulipwa fidia pindi majanga yanapotokea. Hivi sasa, watoa huduma mbalimbali wa bima wamebuni bidhaa mbalimbali za bima ili kuwavutia watumiaji wengi. Natumia fursa hii kuwakumbusha wananchi wote kuchangamkia fursa hii kikamilifu ili kupunguza athari” ameongeza.

Saqware ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Awamu ya Sita Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi nchini kujingua na bima huku akiongeza kuwa ukuaji wa sekta ya bima utasaidia katika kukuza maendeleo ya nchini kwa ujumla.

“Kwa hivi karibuni, suala la bima limekuwa sehemu muhimu ya hotuba za Rais Samia na msisitizo wake mkubwa ukiwa bima ya afya kwa wote. Kama mamlaka, tutajitahidi kuhakikisha ukuaji wa matumizi ya huduma za bima kila mwaka na ili hili lifanikiwe, watoa huduma za bima hawana budi kutoa huduma kwa gharama nafuu” ameongeza.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja amesema utafiti wa awali uliofanywa na mamlaka za wilaya hiyo ulibaini kuwa maporomoko ya matope katika wilaya hiyo uliathiri mamia ya wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) wanaofanya shughuli zao wilayani humo.

“Kiwango cha elimu kuhusu huduma za bima katika wilaya yetu bado kiko chini sana. Hakuna aliyewahi kufikiria kuwa wilaya yetu ingekumbwa na janga kama hili. Tukio hili linatoa somo kwetu sote na tunatakiwa kuanzisha utamaduni wa kutumia bidhaa mbalimbali za bima zinazopatikana kama tunataka kusonga mbele” Amesisitiza Mayanja.

Hapiness Mlay (47) mkazi wa Katesh ambaye ni mmoja wa wanufaika wa fidia hiyo amesema, “Nimefarijika sana baada ya kupata uthibitisho kwamba nitapokea fidia ya shilingi milioni 28.5. Nimekuwa na msongo wa mawazo mkubwa kwa zaidi ya wiki nne tangu mafuriko kutokea hapa. Nachukua fursa hii kuwakumbusha wafanyabiashara wenzangu kupunguza hatari za biashara zao kwa kukata bima, “amesema.