Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekutana na wateja wake wakubwa yaani makampuni na taasisi mbali mbali (Corporates) wa jijini Mwanza ili kujadili fursa za biashara, kutambulisha huduma mpya za benki hiyo sambamba na kuwaejengea uelewa zaidi wateja hao kuhusu faida na manufaa ya huduma hizo.
Benki hiyo pia ilitumia fursa hiyo kujadili na wateja hao namna inavyoweza kuboresha huduma zake kulingana na mahitaji yao.
Akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kupitia timu yake ya Biashara na Uwekezaji (CIB) mwisho wa wiki hii jijini Mwanza, Mkurugenzi wa wateja wakubwa, taasisi binafsi na za serikali kutoka NBC , James Meitaron amesema tukio hilo ni muendelezo wa matukio kama hayo mahususi kwa wateja wakubwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo Dodoma na Arusha.
“Tukiwa kama muhimuli muhimu wa utoaji wa huduma za kifedha nchini, NBC tunatambua umuhimu wa utoaji wa huduma bora kwa wateja na kukuza ushirikiano kati yetu na wateja wetu. Hii inasababishwa na mabadiliko yanayotokana na ubunifu na maendeleo ya kiteknolojia.’’
”Hivyo hatua hii ya kukutana na wateja wetu wakubwa inatoa fursa kwetu kuelezea maboresho makubwa tuliyofanya kwenye huduma zetu sambamba na kutambulisha huduma mpya zilizorahisishwa zaidi kidigitali na zinazoendana na mahitaji ya wateja wetu hususani hawa wakubwa.’’ Amesema
Aidha, kupitia mpango huo benki hiyo imekuwa ikielezea mikakati yake mipana inayolenga kuwahudumia kwa ufanisi zaidi wateja hao, kuwajengea mitandao ya kibiashara miongoni mwao sambamba na kuwasogezea huduma za kibenki karibu zaidi huku huduma ya NBC Connect ikitajwa kama suluhisho muhimu katika kuwasogezea huduma za kibenki wateja hao wakubwa yakiwemo mashirika na kampuni binafsi, pamoja na taasisi za serikali.
“Tunaamini kuwa msingi wa huduma za kipekee ni kuelewa mahitaji na matakwa ya wateja wetu, ziara hizi zinatupatia mitazamo au maono yatakayosaidia kuwa wabunifu na kuboresha uzoefu wa kibenki kwa ujumla.” Ameongeza Bw Meitaron.
Meitaron ametaja baadhi ya mambo muhimu ambayo benki hiyo imekuwa ikiyanzingatia katika kukuza ushirikiano na taasisi za kibiashara hapa nchini kuwa ni pamoja na utoaji wa suluhisho zenye ubunifu katika huduma za kifedha, Ubunifu wa kiteknolojia, Ubia wa kimkakati, Kukuza Ukuaji wa Uchumi pamoja na Uwajibikaji kwa jamii huku kipaumbeke kikiwekwa zaidi kwenye masula ya Elimu, Afya na uhifadhi wa mazingira.
“ Hivyo basi NBC tunazialika jumuiya za wafanyabiashara kuangalia fursa na faida za kushirikiana na taasisi ya fedha ambayo ina dhamira ya dhati na mafanikio yao, kwa kukuza ushirikiano na kutoa zana zinazohitajika katika ukuaji. NBC inalenga kuwa mshirika mwaminifu anaayetegemewa katika biashara hapa nchini,’’ amebainisha.
Hata hivyo Fainess Jeremiah ambaye ni Meneja wa mauzo tawi la Mwanza nae ameeleza kuwa “NBC imerahisisha maisha hasa kwenye upande wa miamala na namna ya upatikanaji wa huduma za kibenki, Hili jukwaa la Nbc ni huduma ya kidigital maalumu kwa ajili ya taasisi na biashara kubwa inayowapa urahisi katika ufanyaji wa miamala. Pia jukwaa hili linamsaidia mteja kuweza kufanya malipo ndani ya nchi kwa TISS ambapo anaweza kulipa mishahara kwa wingi na pia anaweza kufanya malipo nje ya nchi”.
Ameongeza kuwa “ Kwa kupitia Nbc connect wateja wetu hawana haja ya kwenda benki kusubiri huduma, Mteja anaweza kujihudumia akiwa mahali popote pale.”
Wakizungumzia hatua hiyo baadhi ya wateja wa benki hiyo mkoani Mwanza wameipongeza benki ya NBC kwa hatua hii muhimu ambayo imewakutanisha wafanyabiashara kutoka taasisi mbalimbali zilizopo mkoani Mwanza.
“Naipongeza sana Benki ya NBC kwa hatua hii muhimu pia niwaombe NBC waweze kupanua wigo zaidi wa kuwafikia wateja hata waliopo nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa huduma zinafika kila mahala”. Amesema Fredrick Otieno Afisa Mkuu wa operesheni Wa kampuni ya jema Africa na jema chemicals.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato