January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NBC Yakabidhi Basi Jipya Lenye Thamani ya Sh ya Mil 450 kwa Klabu ya KMC, RC Makalla Apongeza

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambae ni mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara, NBC Premiere League hii leo imekabidhi basi jipya kwa timu ya KMC FC ya Kinondoni jijini Dar es Salaam inayoshiriki ligi hiyo huku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw Amos Makalla akionesha kuguswa na jitihada za benki hiyo katika kuboresha ligi hiyo.

Hafla ya makabidhiano ya basi hilo lenye thamani ya sh ya milioni 450 lililotolewa kama mkopo kutoka benki ya NBC imefanyika jana jijini Dar es Salaam na kuhudhuliwa na wadau mbalimbali wakiongozwa na RC Makalla,  viongozi wa Shirikisho la Mpira Miguu nchini (TFF), viongozi na wafanyakazi wa Benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw Theobald Sabi pamoja na viongozi wa Manispaa ya Kindondoni wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Bw Saad Mtambule.

Akizungumza kwenye hafla hiyo RC Makalla, aliipongeza benki hiyo kwa jitihada zake za kuiboresha ligi hiyo kimataifa huku akitoa wito kwa vilabu mbalimbali nchini kuitumia vema benki ya NBC kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo mikopo ya usafiri na Bima kwa wachezaji na benchi la ufundi.

“Kila mtu sasa ni shuhuda wa namna ambavyo ligi yetu imekuwa bora hata kimataifa tangu kuanza kwa udhamini wa NBC. Inafurahisha zaidi kuona udhamini huo hauishii tu kwenye ligi pekee bali pia benki inaguswa na changamoto za timu moja moja…hongereni sana NBC. Naomba sana timu nyingine pia ziige mfano huu wa KMC bila kujali ukubwa wao.’’ Alisema huku akitoa wito kwa uongozi wa timu hiyo kuhakikisha wanarejesha mkopo huo kwa wakati.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw Theobald Sabi alisema hatua hiyo imekuja kufuatia kikao baina ya benki hiyo na vilabu vyote vinavyoshiriki ligi hiyo ikiwemo Klabu ya KMC na kuunda fursa wezeshi za kusaidia timu kujikwamua na changamoto mbalimbali zinazozikabili timu hiyo ikiwemo ya usafiri wa uhakika.

“Ligi hii inahusisha suala zima la usafiri kwa vilabu husika na wakati mwingine timu zinasafiri kwa umbali mrefu sana na hivyo kusababisha uchovu kwa wachezaji. Upatikanaji wa mabasi mazuri ya kisasa utasaidia kupunguza uchovu kwa wacheza ili waweze kuleta ushindani unaohitajika wakiwa viwanjani.Leo hii tumeanza na KMC ila bado vilabu vingine vinafuata,’’ alibainisha Sabi.

Kwa mujibu wa Bw Sabi ukosefu wa vyombo vya usafiri maalum kwa ajili ya timu zinazoshiriki ligi hiyo imekua  ni moja ya chanzo cha vikwazo vingi katika gharama za uendeshaji na utendaji wa timu husika.

 â€œZaidi pia  NBC tunaendelea kushirikiana kampuni washirika wa huduma za  Bima wa Sanlam na Britam  inatoa huduma za bima za afya na maisha  kwa wachezaji  wote wa timu zinashiriki ligi kuu ya NBC , mabenchi ya ufundi pamoja na familia zao.’’ Alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw Saad Mtambule pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa mkopo huo aliihakikishia kuwa wamejipanga kuhakikisha kwamba unarejeshwa kwa wakati huku pia akiahidi kulitunza vyema basi hilo.

Akizungumzia ujio wa basi hilo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe Songoro Mnyonge alisema limepatikana wakati muafaka  na kwamba litamaliza kabisa changamoto ya usafiri iliyokuwa ikiikabili klabu hiyo pale inapohitaji kucheza mechi za mikoa ya mbali.

“Kupitia usafiri huu sasa tuna uhakika wa kusafirisha wachezaji wote na benchi la ufundi sambamba na baadhi ya mashabiki kwenda kwenye mechi zetu nje ya mkoa. Tunahidi kurejesha mkopo huu ndani ya mwaka mmoja kama tulivyokubalina na NBC’’ alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw Amos Makalla (wa pili kushoto) sambamba na  Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw Theobald Sabi (kushoto), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bi.Hanifa Hamza  (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw Saad Mtambule  wakiwa ndani ya basi jipya lililotolewa na benki ya NBC kwa njia ya mkopo kwenda kwa timu ya KMC FC ya Kinondoni jijini Dar es Salaam inayoshiriki ligi Kuu ya Tanzania ili kuisaidia timu hiyo kukabiliana na changamoto ya usafiri. Hafla ya makabidhiano ya basi hilo ilifanyika jijini Dar es Salaam jana.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw Amos Makalla (wa pili kushoto) akipokea mfano wa ufunguo wa gari kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw Theobald Sabi (kushoto) ikiwa ni ishara ya kukabidhiwa basi jipya lililotolewa na benki hiyo kwa njia ya mkopo kwenda kwa timu ya KMC FC ya Kinondoni jijini Dar es Salaam inayoshiriki ligi Kuu ya Tanzania ili kuisaidia timu hiyo kukabiliana na changamoto ya usafiri. Wengine ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw Saad Mtambule (wa tatu kushoto), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge (wa tatu kulia) Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bi.Hanifa Hamza (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa wateja Wadogo wa NBC,Bw  Elibariki Masuke  (Kulia). Hafla ya makabidhiano ya basi hilo ilifanyika jijini Dar es Salaam jana.

















Â