Na Mwandishi Wetu, TimesMajira, Online Kyela
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Japhet Justine, ameongoza ujumbe wa benki kutembelea Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya katika juhudi za kuongeza tija kwenye fursa za kilimo, uvuvi na ufugaji wilayani humo.
“TADB inaazimia kuwezesha wakulima katika wilaya ya Kyela kuongeza tija katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji. Tungependa wilaya kujipanga na kuainisha miradi isiyopungua mitatu itakayowawezesha vijana na wanawake katika minyororo ya thamani katika sekta zote hizi.” amesema Justine wakati akielezea dhima ya ujumbe wa TADB wilayani humo.
Akizungumzia fursa za kilimo wilayani humo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Claudia Kitta, amesema kuwa wilaya ya Kyela ina fursa kubwa katika zao la kakao ambalo karibu kila mwanachi wa walayani humo amepanda miti ya zao hilo.
“Changamoto kubwa ni namna ya kuwezesha wananchi kunufaika na zao hili zaidi kwa kuwa mara nyingi madalali maarufu kama ‘Njemke’ wamekuwa wakitumia mwanya wa ukosefu wa mitaji ya kutosha katika vyama vya msingi,” amesema Kitta.
Ameendelea kusema, “Hii inasababisha wakulima wetu wengi kuuza kwa faida ndogo sana kwa madalali ambao wao huenda kuuza kwa faida mara mbili zaidi. Hii inakatisha tama wakulima.”
Katika kuangazia changamoto ya zao la kakao, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB amesema benki hiyo iko tayari kuwezesha mitaji kwa vyama vya msingi Wilayani Kyela ili waweze kununua nakulipa wakulima kwa wakati.
“TADB ni taasisi ya kifedha kwa maendeleo ya wananchi. Ni azma yetu kuongeza tija katika zao hili lenye thamani kubwa na uhitaji katika soko la dunia.
Ninafahamu kuwa kwa mwaka 2020 pekee pamoja na changamoto ya janga la Corona, wakulima kupitia vyama vya msingi 69 wilaya ni hapa, waliweza kuuza zaidi ya tani 10,000 ya kakao yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 50 kwa tani,”ameelezea Justine.
“Hii ni ishara kubwa kuwa kilimo cha Kakao ni fursa kubwa kwa uchumi wa taifa na kwa TADB kuweza kuchagiza katika kilimo hiki, tutaweza kuongeza kipato cha wakulima wote hawa,” Mkurugenzi huyo amesisitiza.
Pamoja na zao la kakao kuwa linaongoza kulimwa zaidi katika bara la Afrika, kwa kuzalisha zaidi ya tani 3,622,000, Shirika la Kimataifa la Kakao linaitaja Tanzania kuwa ya 24 duniani katika uzalishaji wa zao hili.
Tanzania huchangia kiasi cha asilimia 0.2 tu ya kakao duniani. Pamoja na kuwa katika nafasi hii, Tanzania inatajwa kushuka kwa uzalishaji wa zao hili. “
“Hivyo, kama benki ya maendeleo ya kilimo,ni jukumu letu kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI) ili kuwezesha upatikanaji wa miche bora ya kakao nakuwezesha upatikanaji wa mitaji ili kuhakikishia upatikanaji wa kipato kwa wakulima. Kwa kufanya hivi tunaamini itahamasisha uzalishaji wa kakao, na kuwezesha pia kuongeza thamani kwa zao hili,”alisema Japhet.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kyela, Ezekiel Magehema, aliuambia ujumbe wa TADB azma ya halmshauri hiyo katika kunufaika na uvuvi kutoka sekta ya uvuvi wa Ziwa Nyasa.
“Ziwa hili lipo hapa, lakini bado changamoto kubwa ni ukosefu wa zana za uvuvi na vifaa vya kisasa. Kutokana na kuwa kina cha ziwa ni kirefu sana, tunahitaji kuwezeshwa kupata zana bora za kisasa za uvuvi ili kuwezesha wavuvi wetu kuvua samaki kwa kiasi stahiki na kuongeza pato la kaya na jamii yetu,” amesema Magehama
Kuelezea namna ambavyo TADB inaweza kwa uhakika kuwawezesha wavuvi, Mkurugenzi wa TADB, alielezea namna ambavyo TADB imekwisha wawezesha wavuvi katika Mkoa wa Mwanza, Mara na Kagera ambapo wamewezeshwa jumla ya sh. 1.48 billioni.
Kiasi hiki kimekwenda katika kuwezesha miundombinu ya ukaushaji dagaa kwa njia ya kisasa, ununuzi wa boti za kisasa, mashine za boti, nyavu bora, kutengeneza vyumba vya kuhifadhi samaki (cold rooms) lakini pia kuwezesha ufugaji wa samaki kwa vizimba Ziwa Victoria.
“Huu ni mfano tu kuwa TADB inaweza na iko tayari kuwawezesha wavuvi. Kazi yetu inategemea sana ninyi viongozi hapa kuanisha miradi ili TADB iweze kugusa kwa upana wake wananchi wengi zaidi. Tunajukumu la kuchangia kuongeza ajira kwa vijana ili kuweza kufikia ajira milioni nane ambazo serikali imeazimia kuzitengeneza.
Hii ni fursa ya kipekee katika Halmashauri kuweza kuandaa miradi itakayotoa fursa za ajira katika kilimo, uvuvi na ufugaji,” amesisitiza Justine.
Pamoja na kuzungumza na uongozi wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB alitembelea chama cha msingi cha Mababu CCF, kilichopo wilayani humo ambacho hujishughulisha na kukausha kakao.
Chama hiki cha msingi huuza kakao kwa kampuni ya Iskinoise iliyoko katika Jimbo la Illinois, Marekani. Chama hiki chenye kuongozwa na mwanamama Mizinara Lutolo kimekwisha pokea tuzo ya utambuzi kutoka Shirika la kimataifa la Kakao kutokana na kakao yao yenye ubora zaidi.
Wilaya ya Kyela ni wilaya yenye ardhi yenye rutuba kwa kustawisha mazao kama vile kakao, mpunga, michikichi. Vile vile wilaya hii inafursa ya ufugaji na uvuvi kupitia Ziwa Nyasa.
More Stories
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto
Walimu S/ Sekondari Ilala wafundwa juu ya maadili ya wanafunzi
Dkt. Samia afungua skuli ya sekondari Misufini, Bumbwini