Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WAKULIMA na wadau wa kilimo kutoka Mikoa ya Tabora. Kigoma na Katavi wameipongeza serikali ya awamu ya 6 kwa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuinua sekta ya kilimo nchini.
Wametoa pongezi hizo juzi kwenye hafla ya uzinduzi wa Ofisi ya Kanda ya Magharibi ya Benki hiyo iliyojengwa Mjini Tabora na kupewa jina la Hassan Wakasuvi House ili kumuenzi aliyekuwa mdau wa ushirika nchini, Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa CCM Mkoani hapa marehemu Hassan Wakasuvi.
Wamesema kuwa kuanzishwa kwa benki hiyo ni fursa muhimu sana kwao kwa kuwa itawarahisishia kupata mikopo yenye riba nafuu ambayo itakuwa kichocheo kikubwa cha kufanya kilimo chenye tija ambacho kitainua maisha yao.
Hussein Buchunguka, mkulima kutoka Mkoani Kigoma ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Kigoma, amesema kuwa benki hiyo imewezesha wakulima wa michikichi kupata mashine za kukamlia mafuta ya mawese.
Aidha ameongeza kuwa baadhi yaov wamewezeshwa kupata mitambo ya kuchakata mazao yatokanayo na zao hilo na kuyasindika jambo ambalo limepelekea wengi wao kuinuka kimaisha kupitia vikundi vyao.
‘Tunaishukuru sana Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa kuwa karibu zaidi na wakulima na kuwawezesha mikopo ya bei nafuu ambayo imekuwa na tija kubwa kwa ustawi wao’, amesema Gwicha Homera, mkulima mkazi wa Tabora.
Mdau wa Kilimo, Abdul Mwilima ambaye ni Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Mafuta ya Mawese, kilichopo Mkoani Kigoma ameshukuru Serikali kwa kuanzisha Benki hiyo ili kuchochea kasi ya maendeleo ya wakulima nchini.
‘Hadi sasa TADB imeshatuwezesha mikopo ya zaidi ya sh mil 600 ambazo zimetusaidia kuboresha kiwanda na kuongeza mitambo hivyo kuongeza uzalishaji wa mafuta, kwa siku tunanunua zaidi ya kilo 144,000 za michikichi’, ameeleza.
Amemshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Kilimo na Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo kwa kusimamia vizuri sekta ya Kilimo na kuhakikisha TADB inawezeshwa mtaji ili kufanikisha malengo yake ya kuwainua wakulima.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Frank Nyabudege amewahakikishia kuwa benki hiyo imeanzishwa kwa ajili yao hivyo akawataka kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa ili kufanikisha shughuli zao.
‘TADB inakua kwa kasi sana, tulianza na mtaji wa sh bil 60 mwaka 2015 baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani alituongezea fedha zaidi, awali alitupatia sh bil 208, baadaye bil 210 na mwaka huu pia katupatia bil 165’, ameeleza.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo Ishmael Kasekwa ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwaongezea mtaji zaidi ili kufanikisha azma yake ya kuinua wakulima nchini.
Amebainisha kuwa mwaka 2020 TADB ilipata faida ghafi ya sh bil 12.6, mwaka 2021 wakapata bil 16, mwaka 2022 bil 15.6 na mwaka jana bil 18.1, kwa mwaka huu faida itaongezeka zaidi, haya ni mafanikio makubwa .
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya sekta ya kilimo nchini ili kuchochea kasi ya uzalishaji mazao mbalimbali.
Amebainisha kuwa Tanzania sasa ni nchi ya pili Barani Afrika kwa uzalishaji wa tumbaku na uzalishaji wa mazao mengine utaendelea kuongezeka zaidi kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya 6.
Amesisitiza kuwa atahakikisha nchi inakuwa na sera nzuri yaf kilimo ili kumuinua zaidi mkulima ikiwemo taasisi za fedha kuwa na mikopo yenye riba nafuu zaidi ambayo haitamwumiza mkulima.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi