December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya EQUITY yazindua huduma ya Live Chat

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Benki ya EQUITY imezindua huduma mpya katika kituo chao Cha huduma kwa wateja iitwayo Live Chat ambayo ni ya kidigitali inayomuwezesha mteja kupata huduma muda wowote masaa 24 mwaka mzima.

Huduma hiyo ambayo imewasogeza karibu zaidi na wateja, itamfanya mteja kuweza kuwasiliana na mtoa huduma wa Benki Moja kwa moja Live na kuweza kupata huduma hapo hapo.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya EQUITY, Isabela Maganga wakati wakiadhimisha wiki ya huduma kwa wateja na kusherehekea pamoja nao katika kutoa huduma kwao.

“Huduma ya Live Chat faida yake kubwa ni kutuweka sisi karibu sana na wateja wetu ambapo mteja na mtoa huduma wanaongea Moja kwa moja Live na kuweza kumpa huduma hapo hapo”

Aidha Maganga amesema Kupitia huduma hiyo, mteja atapata faida ya kurahisisha muda wake wa kutosubiri kupata huduma kwa muda mrefu ambapo akishaingia hewani mteja anakutana na mtoa huduma hapo hapo.

“Mteja anapata ujuzi wa tofauti na kupiga simu,
mteja akipiga simu huwa anakaa kidogo anasubiri mpaka mtoa huduma apokee lakini Live chat yenyewe haina kusubiri akiingia online anamkuta tayari mtoa huduma yupo , wanaongea, anatatua na anampa solution Moja kwa moja” Alisema Maganga na kuongeza kuwa

“Hii inasaidia sanasana kwa wale ambao Wana simu janja katika kufanya mawasiliano kidigitali na kutumia huduma za kibenki papo kwa papo”

Kadhalika Maganga amesema Benki ya EQUITY imewekeza kwenye njia nyingi sana za kimtandao za kidigitali, ambapo mpaka sasa asilimia 88 ya wateja wao wanahudumiwa kwa mifumo ya kidigitali kwa kutumia simu za mikononi, Kompyuta lakini pia kwa kutumia website.

“Mteja akiwa na simu yake ndiyo Benki yake, akiwa na kompyuta yake ndiyo Benki yake, akiingia kwenye mtandao wowote anakutana na Benki yake na Benki yake ni EQUITY”

Maganga amesema Kituo chao cha huduma kwa wateja wanazidi kukipanua na kuongeza huduma zaidi ili wao waendelee kuwa karibu zaidi na wateja wao na kuendelea kutoa huduma kwa muda wote asubuhi mpaka usiku.

“Nawakaribisha sana wateja wetu Equity na pia nawashurku kwa kutuamini sisi ambao tunawapa huduma za kibenki na pale tunapokua tunatimiza malengo yao ya shughuli zao za kiuchumi na kijamii”

Kwa upande wake Meneja wa Tawi la Mwenge, Magreth Makundi ameahidi kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora kwa kiwango Cha juu kabisa na kuwaahidi wateja wao wote na kuendelea kupata huduma bora zaidi.