Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Benki ya CRDB imeingia makubaliano ya uwezeshaji wajasiriamali wadogo na wakati (MSMEs) wenye thamani ya Shilingi bilioni182 na shirika la fedha la nchini Ufaransa la Proparco.
Makubaliano hayo ambayo yanajumuisha mkopo na dhamana za mikopo kwa wajasiriamali, itasaidia kuwawezesha wajasiriamali nchini sambamba na mpango wa maendeleo wa Taifa, kwa kuzingatia zaidi wajasiriamali wanawake, wajasiriamali katika sekta ya kilimo, pamoja na wajasiriamali ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa na janga la UVIKO-19.
Proparco, ni kampuni tanzu ya shirika la maendeleo la Ufaransa Agence Française de Développement Group (AFD Group), ambalo limejikita katika kutoa ufadhili na usaidizi kwa biashara na taasisi za kifedha barani Afrika, Asia, Amerika Kusini na Mashariki ya Kati.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema ushirikiano huo umekuja wakati muafaka na utasaidia kwa kiasi kikubwa kufufua sekta ya ujasiriamali nchini na kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Nidhahiri kuwa katika kipindi cha mitatu iliyopita wajasiriamali wengi wameathirika na janga la UVIKO-19. Tunatarajia kuwa fedha pamoja na dhamana hizi tunazozipata leo, pamoja na huduma zetu bunifu kwa ajili ya wajasiriamali, zitasaidia kuwainua na kuwawezesha wajasiriamali nchini kuboresha biashara,”amesema
NsekelaNsekela alisema Benki ya CRDB imesaini mikataba mitatu na Proparco ambapo mkataba wa kwanza unajumuisha Shilingi 115 bilioni ambazo zitaelekezwa kusaidia sekta ya kilimo.
Fedha hizi zitatumika kuwawezesha wakulima wadogo na wakati kufanya kilimo cha kisasa na stahimilivu kwa gharama nafuu ili kuongeza uwezo wa sekta hiyo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkataba wa pili umehusisha Dhamana ya Mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 20 kwa ajili ya uwezeshaji wa wajasiriamali walioathirika na janga la UVIKO-19.
Nsekela mesema dhamana hiyo ya mikopo itawezesha kuwainua wajasiriamali wengi walioathirika na kutoa matumaini mapya katika biashara zao.
Dhamana hiyo ni sehemu ya mpango wa uwezeshaji unaotekelezwa na Serikali ya Ufaransa kupitia program ya ‘Choose Africa’ inayotekelezwa na AFD.
Mkataba wa tatu umehusisha Dhamana ya Mikopo ya EURIZ yenye thamani ya Shilingi bilioni 47 kwa ajili ya uwezeshaji wa wajasiriamali wanawake nchini. Dhamana hiyo inaambatana na mafunzo kwa wajasiriamali wanawake ili kusaidia kuboresha biashara zao.
Dhama hiyo ya Mikopo ya Euriz inawezeshwa kwa kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya (EDF), Jumuiya ya Nchi za Carribean na Pacific (OCPAZ).
Katika maelezo yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Proparco, Gregory Clemente alibainisha kuwa fedha na dhamana hizo zilizotolewa zitachangia kwa kiasi kikubwa malengo ya programu ya Chagua Afrika, mpango wa uwezeshaji wajasiriamali Afrika unaotekelezwa na Serikali ya Ufaransa uliozinduliwa mwaka wa 2018.
“Proparco inafuraha kuanzisha uhusiano huu na Benki ya CRDB na kuikaribisha kama mshirika mpya wa mpango wa Chagua Afrika. Hatua hii ya kusaini mikataba inaonyesha dhamira ya Proparco kwa wajasiriamali wa Tanzania, na ni matumaini yetu ushirikiano huu utaiongezea uwezo Benki ya CRDB katika uwezeshaji wajasiriamali kupitia mikopo nafuu,” alisema Clemente.
Benki ya CRDB inaongoza katika juhudi za kusaidia wajasiriamali nchini Tanzania kupitia huduma na bidhaa bunifu zinazotolewa na benki hiyo. Kupatikana kwa fedha na dhamana hizo kutaisaidia Benki ya CRDB kuongeza uwezo wake katika kuwawezesha wajasiriamali nchini jamba ambalo litasaidia kuchochea ukuaji endelevu, kukuza ajira, ujuzi na uzalishaji mali nchini.
More Stories
Mwalimu adaiwa kumfanyia ukatili mwanafunzi
NAOT watakiwa kuendana na viwango vya ukaguzi
10 Best Online Internet Casinos For Real Cash Oct 202