March 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bechina atoa futari kwa wananchi 750 Ilala

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wananchi 750 wa Mtaa wa Kalume, wakiwemo wenye mahitaji maalum, wamenufaika na msaada wa futari uliotolewa katika mwendelezo wa jitihada za kijamii za kusaidia makundi mbalimbali wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Katika hafla hiyo ya ugawaji wa futari, mgeni rasmi alikuwa Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ally Ngeruko, ambaye alishiriki kushuhudia utoaji wa msaada huo kwa wananchi.

Akizungumza baada ya kukabidhi futari hiyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kalume, Hajji Bechina amesema mtaa huo una idadi kubwa ya wafanyabiashara, na kwa kushirikiana na uongozi wa mtaa, wameanzisha utaratibu wa kusaidia jamii kwa kugawa chakula katika kipindi cha Ramadhani.

Amesema msaada huo unahusisha utoaji wa chakula kwa wananchi pamoja na kuwasaidia wenye mahitaji maalum, na kuongeza kuwa pia wamekuwa wakitoa msaada wa sanda na fedha kwa ajili ya kusaidia gharama za mazishi kwa familia zenye uhitaji.

Amesema thamani ya futari iliyogawiwa ni shilingi milioni 17, na kwamba wananchi wengi wenye kipato cha chini wamenufaika na mpango huo wa kijamii.

Diwani wa Kata ya Ilala, Saady Kimji, amempongeza Mwenyekiti Bechina pamoja na uongozi wake kwa kuanzisha utaratibu wa kugawa futari kila mwaka na kuendelea kusaidia jamii.

Aidha, Kimji amesema Kata ya Ilala inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya misikiti na kudumisha amani, akisisitiza ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa serikali, vyama vya siasa na taasisi za kidini, na amewataka viongozi wengine wa mitaa kuiga jitihada hizo ili kuimarisha mshikamano wa kijamii.

Kwa upande wake, Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ally Ngeruko amesema utoaji wa sadaka na kusaidiana katika jamii ni muhimu kwa ustawi wa jamii, akihimiza wananchi kuendeleza mshikamano, kusaidiana na kushirikiana katika mambo ya kijamii kwa mujibu wa mafundisho ya dini.