December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bashungwa:Serikali kuwezesha kundi la machinga kwa mkopo nafuu kutoka Serikali ya India

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Innocent Bashungwa amesema kuwa serikali kupitia wizara ya Fedha na Mipango ipo katika mazungumzo na serikali ya India ili kupata mkopo wa Dolla za Kimarekani milioni 30  utakao tumika kuwezesha machinga hapa nchini.

Waziri Bashunga,ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha Jukwaa la Maendeleo ya sekta ya Fedha ambacho pia kililenga kujadili na kuweka mikakati ya serikali kuliwezesha kundi hilo.

“Hivi sasa Serikali  kupitia wizara yetu ya Fedha na Mipango ipo kwenye mazungumzo hayo ya  kupata mkopo huo wenye masharti nafuu wa dola za kimarekani milioni 30 ambazo zitatumika kuwezesha machinga hapa nchini”amesema Bashungwa

Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum

Aidha amewaagiza Makatibu wakuu wa Wizara za Kisekta kukutana haraka mara baada ya kikao hicho ili kujadili changamoto pamoja na fursa zilizopo kwa kundi hilo la machinga.

 “Nawaagiza Makatibu Wakuu wa Wizara za kisekta katika eneo hili tukiwemo sisi  TAMISEMI,Wizara ya Fedha na Mipango,Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum mkutane haraka ili mjadili changamoto na fursa wanazokabiliana nazo machinga hapa nchini ili serikali iweze kuzifanyia kazi.”amesema Bashungwa

Vile vile amewaagiza viongozi hao kutafuta mapendekezo na kuja na majibu yatakayo jibu changamoto za kundi hilo lakini  pia kuona ni vitu vinavyoweza kukwamisha mikakati na jitihada za zinazofanywa na serikali.

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum

Kwa mujibu wa Bashungwa ,Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuliwezesha kundi la machinga kwa kuboresha na kuweka mazingira rafiki ya kufanya biashara.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis,amemshukuru Rais Samia kwa namna ambavyo anaendelea kuliinua kiuchumi kundi hilo.

Naibu Waziri huyo amesema, kutokana na umuhimu huo Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa kundi la machinga linahudumiwa kwa upekee kwa kuratibu shughuli wanazozifanya ili ziweze kuwanufaisha na kuwaletea maendeleo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt.Lawrence Mafuru

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango  Lawrence Mafuru, amesema kuwa Wizara yake ipo katika hatua za kutengeneza Bajeti Kuu ya Serikali, alisema miongoni mwa vipaumbele katika bajeti hiyo ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan angependa kuviona ni pamoja na sekta ambazo zinazalisha kama Kilimo, mifugo, uvuvi na nishati lakini pia wamachinga.

Mafuru amesema kuwa warsha ya wamachinga itasaidia kutoa fursa ya kujifunza lakini pia kuwa na sera itakayoelekeza rasilimali fedha kutoka kwa wadau mbalimbali inapatikanaje kwa ajili ya eneo hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa shirikisho la machinga nchini (SHIUMA) Ernest Masanja,ameipongeza  serikali kwa namna ambavyo inaweka mazingira rafiki kwa wamachinga.