Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameuagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kumuondoa Mkandarasi wa kampuni ya Kay Bouvet Engineering Ltd ya nchini India na kumtafuta Mkandarasi mwingine mwenye uwezo na sifa za kujenga miundombinu ya barabara katika Kiwanda cha sukari cha Mkulazi Mkoani Morogoro.
Waziri Bashungwa ameeleza hayo wakati akikagua ujenzi wa kiwanda na miundombinu ya barabara katika Kiwanda cha Sukari na Shamba la Mbigiri na kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mkandarasi huyo.
“Jukumu la TANROADS ni kusimamia ujenzi wa kiwanda hiki katika miundombinu ya barabara lakini Mkandarasi huyu ni mbabaishaji, na tumeamua kumuondoa kwa kuwa hana mitambo ya kutosha ya kutekeleza kazi ya ujenzi wa barabara pia hana sifa na uzoefu wa barabara kwa kiwango cha lami”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kutangaza zabuni ya mradi huo mara moja na kumpata Mkandarasi mwenye sifa na uwezo wa kutekeleza kwa ufanisi mkubwa na kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Bashungwa amesema kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya kiwanda hicho kilichofikia asilimia 70 kutasaidia kuongeza uzalishaji wa sukari nchini na kulisaidia Taifa kuzalisha sukari ya kujitosheleza kupitia Viwanda vya ndani.
Vilevile, Bashungwa ameuagiza uongozi wa Kiwanda kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kumsimamia Mkandarasi wa ujenzi wa Kiwanda hicho ili ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi 2024 ujenzi wa kiwanda hicho uwe umekamilika kwa asilimia 100.
Waziri Bashungwa, amemshukuru Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya Ujenzi wa viwanda nchini ikiwa ni pamoja na kiwanda cha Sukari cha Mkulazi ambacho kitakiwa na uwezo wa kusaga tani 2500 za miwa na kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka.
Akitoa taarifa Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Kyamba amesema TANROADS ina jukumu la kusimamia kazi zote za manunuzi, ujenzi wa kiwanda, majaribio na shughuli zote za ukamilishaji wa kiwanda na kuanza uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho cha Mkulazi.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema Mkandarasi anayetekelza ujenzi wa miundombinu ya barabara amekuwa akisua sua na kupelekea shughuli za uzalishaji wa kiwanda hicho kutokufanyika kwa ufanisi, kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara zinazounganisha kiwanda na Mashamba ya miwa.
More Stories
Rehema Simfukwe atoboa siri sababu kuimba wimbo wa Chanzo
Tanzania ipo tayari kupokea wakuu wa nchi,mkutano wa nishati-Dkt.Kazungu
Chunya yafikiwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano