February 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Barrick yaichangia Serikali trilioni 3.6 kwa kipindi cha miaka minne

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Barrick imechangia kiasi cha shilingi trilioni 3.6 katika Mapato ya Serikali kupitia kodi, mrabaha, na tozo mbalimbali kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2024.

Hayo yameelezwa leo Februari 13, 2025 Jijini Dodoma na Meneja Mkaazi wa Kampuni hiyo hapa nchini Dkt. Melkiory Ngido mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati akiwasilisha Maendeleo ya Kampuni Tanzu Baona ya Barrick Gold na Serikali ya Tanzania inayofamika kama Twiga Minerals.

Dkt. Ngido ameelezea kuwa, kwa mujibu wa takwimu za miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2024, Kampuni Barrick imewekeza zaidi ya dola bilioni 4.24 (Tsh trilioni 11) katika shughuli zake ndani ya nchi, huku dola bilioni 1.5 (Tsh trilioni 3.6) zikilipwa serikalini kupitia kodi, mrabaha, na tozo mbalimbali.

Amesema kuwa, Kampuni ya Barrick ilipochukua usimamizi wa shughuli zake nchini Tanzania mnano mwaka 2019, kampuni hiyo imeendelea kuwa mdau mkubwa wa uchumi kupitia uwekezaji, ajira, na miradi ya kijamii.

Mchango wa Kiuchumi

Dkt. Ngido ameelezea kuwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 158 (shilingi bilioni 412.4) sawa na asilimia 4 zimelipwa kama gawio la Serikali kutoka na ubia huo.

Sambamba na hilo, Dkt. Ngido amesema kiasi cha Dola bilioni 2.3 (shilingi trilioni 6.04) sawa na asilimia 55 ya matumizi yote yameelekezwa kwa wasambazaji wa ndani, huku asilimia 32 ya uwekezaji huo kiasi cha dola bilioni 1.37 (shilingi 3.57) kimelipwa kama kodi, mrabaha, na tozo mbalimbali kwa serikali.

Ameongeza kuwa, kiasi cha dola milini 397 milioni (shilingi trilioni 1,03) sawa na asilimia 9 zimetumika kulipa mishahara ya wafanyakazi huku dola milioni 30 (shilingi bilioni 78.3) zikitumika kwenye utafiti wa madini katika maeneo hayo na kiasi cha dola milioni 15.6 sawa na shilingi bilioni 40.7 zimeelekezwa kwenye miradi ya kijamii.

Ajira kwa Watanzania

Dkt. Ngido amesisitiza kuwa, Barrick imejidhatiti katika kutoa ajira kwa Watanzania, ambapo asilimia 96 ya wafanyakazi wake ni raia wa Tanzania, ambapo hivisasa, Kampuni ina wafanyakazi 6,185, kati yao 5,933 ni Watanzania, huku wageni wakibaki asilimia 4 pekee na kwamba asilimia 53 ya wafanyakazi hao wametoka kwenye jamii zinazozunguka migodi.

Ameongeza kuwa, asilimia 100 ya nafasi za juu za usimamizi zinashikiliwa na Watanzania huku uwakilishi wa wanawake wanawakilisha ukiwa ni asilimia 13 ya wafanyakazi wote na kwamba Barrick inazidi kuimarisha mchango wake kwa Tanzania, kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya madini, kuinua wajasiriamali wa ndani, na kuboresha maisha ya jamii zinazozunguka migodi yake.

Ikumbukwe kuwa, Ripoti ya 14 ya Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) iliyochapishwa mwezi Juni 2024 ilithibitisha kuwa Kampuni ya Barrick Tanzania ilichangia asilimia 51 ya Mapato ya Serikali yote yaliyotokana na tasnia ya uziduaji, ikiwa ni mchangiaji mkubwa kama taasisi moja katika uchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt. Mathayo David ameipongeza Kampuni hiyo kwa juhudi hizo huku akitoa wito kwa watendaji na wafanyakazi wa Kitanzania walioajiriwa katika Kampuni hiyo kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa ili kulinda imani ya Kampuni pamoja na sifa ya taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Madini, Kamishna Msaidizi Uendelezaji wa Madini na Migodi kutoka Wizara ya Madini Mhandisi Ally Samaje amesema kuwa Serikali inajivunia kwa mafanikio makubwa ya Kampuni Tanzu baina ya Barrick na Serikali ya Twiga Minerals na kwamba mazungumzo ya kuanzisha Kampuni zingine za ubia kati ya Serikali na wawekezaji wengine yako katika hatua nzuri.