November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baraza la vyama vya siasa lampa 5 Samia

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

VIONGOZI wa vyama vya siasa nchini wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuondoa zuio la mikutano ya hadhara ambalo limekuwepo tangu mwaka 2016.

Viongozi hao wametoa pongezi hizo ikiwa ni siku mbili baada ya Rais Samia kutangaza ruhusa ya mikutano ya hadhara huku akiwahimiza wanasiasa kuzingatia katiba, sheria, mila na desturi za nchi.

Mbali na suala la mikutano ya hadhara, Rais Samia alieleza pia kuhusu mabadiliko ya sheria zinazosimamia vyama vya siasa pamoja na mpango wa kuukwamua mchakato wa katiba.

Akizungumza na vyombo vya habari jana,Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu alisema ameitisha mkutano huo wa baraza la vyama vya siasa kwa dharura lengo ikiwa ni kutoa pongezi kwa Rais Samia kwa jambo kubwa ambalo amelifanya juzi.

Alisema Rais Samia ameonesha ukomavu kwa kuwaleta pamoja viongozi wote wa vyama vya siasa kikiwemo CHADEMA ambacho kimekuwa kikisusia mikutano mingi ya Baraza na Kitaifa.

“Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka, tukae pamoja, tushindane kwa hoja. Ninamuahidi Rais wetu kwamba chama chetu cha Ada-Tadea pamoja na Baraza zima, tutampa ushirikiano wa kutosha,” alisema na kuongeza;

“Vikao vingi vikifanyika na matukio mengi ya kitaifa yakifanyika wenzetu walikuwa wanajitenga hatukuwa tunafurahishwa ni jambo hilo ambalo lilituumiza moyoni kabisa.’’alisema Khatibu.

Aidha alisema hata juzi Rais Samia tumeona hisia zake hakuwa hakifurahishwa na tukio hilo la vyama kususa vikao, ila ameweza kuonesha uwezo mkubwa na uzalendo wa kujishusha kuzungumza na watanzania wenzetu Chadema na ndio siasa tunayoitaka katika taifa letu.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba alisema anampongeza Rais Samia kwa kutembea katika maneno yake ya R nne zinazohusu maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kuijenga upya nchi hii.Alisema Rais Samia ametumia busara za kiuongozi kurudisha mikutano ya hadhara ambayo ni haki ya vyama vya siasa kikatiba na kisheria.

“Huu ni uamuzi mzuri wa kupongeza, kinachotakiwa ni kutekeleza kwa sababu muda ni mfupi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu,” alisema Profesa Lipumba.Alisema tukio la juzi la Rais Samia kuwaita viongozi wa vyama vyote vyenye usajili 19 na wote kuhudhuria Ikulu ni tukio la na kihistoria.

‘’Katika awamu zote hizi hakuna Rais ambaye amekutana na kuita viongozi wote wa vyama vya siasa na kukutana nao Ikulu kwa ajili ya mazungumzo, hili ni tukio la kwanza tangu mfumo wa vyama vingi kuweza kuanza nchini,’’alisisitiza.

Alisema zuio hilo lililoanza mwaka 2016,Rais Samia ameliondoa rasmi ni jambo jema pamoja ya kuwa ni haki ya sheria na kikatiba .

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, Joseph Selasini alisema anaamini uamuzi alioufanya Rais Samia hautawafurahisha baadhi ya watu hasa ndani ya chama chake.

“Siamini kama watu wote ndani ya chama chake wanamuunga mkono katika hili. Lakini, uamuzi wenye busara hauhitaji kuungwa mkono na watu wengi.”

Aliwashangaa baadhi ya watu wanaodhani kumpongeza Rais ni kuua upinzani. Alisema jambo alilofanya Rais Samia lilikuwa ni gumu, hivyo anahitaji pongezi ili kumtia moyo katika kuimarisha demokrasia hapa nchini.

Mwenyekiti wa Chama Cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamadi Rashid alisema uamuzi wa Rais kufungua mikutano ya hadhara umefungua haki ya kikatiba ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.

“Jana (Juzi), Rais amewawezesha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka na kusikiliza sera za vyama mbalimbali kupitia mikutano ya hadhara,” alisema.