Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline.
MWENYEKITI wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo amelipongeza Baraza hilo kwa kazi nzuri ya kupambana na changamoto ya ajali za barabarani nchini kupitia mikakati, ushauri, na dhamira safi ya kuhakikisha kuwa ajali zinapungua kwa kiasi kukubwa na hatimaye kumalizika kabisa.
Akizungumza kwenye Kikao cha Usalama barabarani Namba 02/2024 kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Golden Tulip Hotel Jijini Dar es salaam Mei 30, 2024 Sillo amepongeza baraza na kuwaahidi ushirikiano mkubwa wakati wowote kwa jambo lolote linalolenga kuboresha baraza hilo na majukumu yake.
“Niwaahidi kama Mwenyekiti wenu kwamba nipo tayari kujifunza kutoka kwenu na kuwapa ushirikiano mkubwa wakati wowote kwa jambo lolote linalolenga kuboresha baraza letu na majukumu yake pia nimshukuru Mhe. Jumanne Sagini (Mb) Naibu Waziri wa Katiba na Sheria kwa kuliongoza vyema baraza tangu alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi natambua kazi zilizofanyika kwa weledi mkubwa na maendeleo tunayoyaona ni dhahiri yamefanywa katika uongozi wake mimi napokea na kuendeleza pale alipoishia pia namuombea na kumtakia kila la heri,”amesema Sillo.
Kwa upande wake aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini (Mb) amekabidhi nafasi hiyo kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa sasa Mhe. Daniel Sillo (Mb) na kuwasisitiza wajumbe wa Baraza kumpa ushirikiano kama alioupata wakati akitumikia nafasi hiyo.
“Naomba nikabidhi nafasi hii kwa Mhe. Daniel Sillo muendelee naye pale nilipoishia pia nawashukuru kwa kuwa mmenijenga, mmeniimarisha na pale nilipokuwa nahitaji msaada wa kiofisi au kazi za nje mlikuwa mnanipatia ushirikiano wa hali ya juu pamoja na mimi kuwa mtiifu katika matumizi ya sheria za barabarani na nyie pia mlikuwa mnafanya kazi kwa weledi ili kupunguza majanga barabarani,”amesema Sagini
Vile vile Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani ambaye ni Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile (Mb) alimshukuru Sagini kwa kipindi chote cha uongozi wake thabiti na usimamizi mzuri akiwa kama Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani katika baraza hilo tumeshuhudia Usafiri wa mabasi kwa Saa 24 ukirejea huku kukiwa na Usalama mkubwa sambamba na mafanikio mengine mengi.
Aidha, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Ramadhani Ng’anzi akimkaribisha Mwenyekiti mpya wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo alimuhakikishia kuwa, watashirikiana vema katika Nyanja zote katika kutekeleza majukumu ya usimamizi wa usalama barabarani na kumtakia majukumu mema mapya aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini (Mb).
Ikumbukwe kuwa Baraza la Taifa la Usalama barabarani ndiyo Chombo chenye dhamana ya kusimamia masuala yote ya kisera yahusuyo Usalama barabarani nchini na Chombo hiki kilianzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 96 cha Sheria ya Usalama barabarani, Sura ya 168 ambapo linaundwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wasiopungua 18 wanaoteuliwa na Waziri mwenye dhamana kwa uratatibu ulivyo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi huwa ndiye Mwenyekiti wa Baraza, Naibu Waziri Wizara ya Uchukuzi huwa Makamu Mwenyekiti na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini huwa Katibu Mtendaji wa Baraza hilo.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba