Na Israel Mwaisaka,Timesmajiraonline, Nkasi
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Nkasi mkoani Rukwa limewafukuza kazi watumishi wawili wa idara ya afya kwa utoro kazini.
Akitoa taarifa ya kufukuzwa kwa watumishi hao baada ya baraza hilo kujigeuza na kuwa kamati mwenyekiti wa halmashauri Pankrasi Maliyatabu aliwataja Watumishi hao kuwa ni Atanasi Mgunda Mteknolojia msaidizi na Japhet Kimondo ambaye ni tabibu msaidizi.
Amesema kuwa Watumishi hao wawili wamekua watoro kazini kwa kipindi kirefu ambapo Atanasi Mgunda yeye ni mtoro kazini tangu Januari 2024 na Japhet Kimondo yeye hajaonekana kazini toka Machi,2024.
Mwenyekiti huyo wa halmashauri aliutumia mwanya huo kuwatahadharisha watumishi wazembe na watoro kuwa watashughulikiwa huku akidai kuwa sheria inaelekeza kuwa mtumishi mtoro kazini shauri lake lianze kusikilizwa ndani ya siku tano za utoro wake na siku 90 afukuzwe kazi.
Mkurugenzi mtendaji wa wilaya Afraha Hassan kwa upande wake alidai kuwa halmashauri yake kwa sasa kati ya mambo inayoyasimamia ni suala la nidhamu kwa watumishi na kuwa na kuwa hicho kilichofanyika cha kuwafukuza watumishi hao ni mwanzo wa usimamizi wa hayo.
Pia alidai kuwa halmashauri imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na kamati juu ya kukaa na maafisa tarafa ili kujua changamoto zao ambapo kubwa ni kutaka kuona viongozi hao wa serikali wanashirikiana vyema na halmashauri katika usimamizi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Huku akifafanua kuwa sehemu ya maagizo hayo ni kutaka magari yote mabovu halmashauri yatengenezwe na kuwa hadi ifikapo Disemba 15 ya mwaka huu magari mengi yatakua yametengenezwa.
Akihitimisha baraza hilo mwenyekiti wa halmashauri hiyo Pankrasi Maliyatabu aliwataka Madiwani wakawe mstari mbele katika kuihamasisha jamii juu ya kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili waweze kupata fursa ya kuwachagua viongozi watakaowaongza katika maeneo yao.
More Stories
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25