November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baraza huru la kusikiliza malalamiko ya wananchi kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu lazinduliwa Mwadui

Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga.

BARAZA Huru litakaloshughulikia malalamiko dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za kibinadamu walivyotendewa wananchi wa vijiji 12 vinavyouzunguka Mgodi wa Almasi wa Mwadui uliopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga limezinduliwa rasmi mkoani Shinyanga.

Baraza hilo limezunduliwa rasmi ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofanyika nje ya Mahakama ya Kimataifa ya nchini Uingereza yaliyoelekeza kuundwa kwa baraza huru litakaloshughulikia malalamiko ya wananchi wanaolalamika kutendewa vitendo vya ukatili na mgodi wa Almasi wa Mwadui.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Joseph Mkude ambaye amemwakilisha mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema amepongeza hatua ya kuanzishwa kwa Baraza hilo huru huku akiwataka wajumbe wake wahakikishe wanatenda haki wakati wote wanaposikiliza malalamiko ya wananchi.

“Nichukue fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru wale wote waliohusika na mchakazo mzima wa uundwa wa Baraza hili, kikubwa tunachowaomba hakikisheni mnatenda haki wakati wote wa usikilizaji wa malalamiko ya wananchi ili lengo lililokusudiwa liweze kutimia,”

“Niwaombe msisite kuwasiliana na Serikali wakati wowote pale patakapojitokeza tatizo lolote kabla mambo hayajaharibika, unesheni uhalisia wa haki kutendeka ili pawe na tija kwa walengwa wenyewe,” ameeleza Mkude.

Msemaji wa Kampuni ya Petra Diamonds Ltd inayomiliki mgodi wa Almasi wa Mwadui (WDL), Richard Duffy amesema kuundwa wa Baraza hilo ni maridhiano kati ya Kampuni mwekezaji na wananchi wanaozunguka eneo la mgodi ambao kwa namna moja ama nyingine walipata madhara.

Duffy amesema mfumo wa uendeshaji wa Baraza hilo huru ni tofauti na mifumo ya uendeshaji wa kimahakama au Serikali ambapo pia amewashukuru wale wote walioshiriki katika uundwaji wake huku akiwaomba wajumbe wake watende haki wakati wote.

Naye Mwenyekiti wa Baraza huru la Usuluhishi, Dkt. Rugemeleza Nshala amesema baraza hilo limeundwa na wajumbe huru ambao hawatokani na mgodi wa Almasi wa Mwadui wala Serikali na kazi yao kubwa itakuwa kuwasikiliza wananchi wote ambao tayari wamesajili malalamiko yao kwenye Baraza.

“Yapo mambo mengi ambayo yamefanyika hadi kufikia hatu ya kuundwa kwa Baraza hili, hili ni Baraza huru na wajumbe wake si waajiriwa wa eneo lolote lile, bali ni huru wanaotakiwa kuyaangalia matatizo yaliyojitokeza na mwisho wa siku waweze kutoa maamuzi,”

“Kuundwa kwa Baraza hili kunatokana na kesi iliyokuwa imefunguliwa kule nchini Uingereza iliyofunguliwa lakini ilimalizika kwa makubaliano ya kuundwa kwa chomba hiki na kwamba wale wote walioguswa na matendo ambayo si mazuri kutoka kwa waliokuwa wanafanya ya ulinzi wa mgodi waweze kusikilizwa na walipwe fidia,” ameeleza Nshala.

Nshala amesema mpaka wakati Baraza hilo linazinduliwa tayari kuna malalamiko ya wananchi yapatayo 5,575 ambayo yameisha sajiliwa na ndiyo yatakayosikilizwa na Baraza na kwamba suala la msingi ni kuona haki za binadamu zinaheshimiwa na ikitokea ukiukwaji basi wahusika waweze kupata haki zao.

Kwa upande wao mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, William Jijimya na Mbunge wa jimbo la Kishapu, Boniface Butondo wameelezea kuridhishwa kwao na uundwaji wa Baraza hilo na kwamba wanaamini wananchi wote waliokuwa wakidai kutendewa vitendo vilivyokiuka haki za kibinadamu sasa watasikilizwa na kupewa haki zao.

“Binafsi niishukuru Serikali yetu ya awamu ya sita ambayo imekuwa ni sikivu kwa wananchi wake, baada ya kusikiliza malalamiko ya wananchi wetu hawa wanaoishi kandokando ya Mgodi wa Mwadui, ikaridhia kuundwa kwa Baraza hili, tunaishukuru sana, kikubwa tuwaombe wajumbe wake watende haki,” ameeleza Jijimya.

Madiwani wa kata za Maganzo, Lwinzi Kidiga na Kata ya Idukilo, Sara Marco ambao kata zao ni miongoni mwa kata zinazozunguka mgodi wa Almasi Mwadui, wameishukuru Serikali kwa kuruhusu Baraza hilo kuundwa ili kusikiliza malalamiko ya wananchi waliotendewa vitendo vya ukiukwaji wa haki za kibinadamu ili waweze kulipwa fidia.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude (kulia) akikata utepe kwenye nyaraka rasmi zenye makubaliano ya uanzishwa wa Baraza huru la kusikiliza malalamiko ya wananchi ikiwa ni ishara rasmi ya kuzinduliwa kwa Baraza hilo, kushoto ni Msemaji wa Kampuni ya Petra Diamonds Ltd inayomiliki mgodi wa Mwadui, Richard Duffy.
Mwenyekiti wa Baraza Huru la kusikiliza malalamiko ya wananchi, Dkt. Rugemaliza Nshala (mwenye shati la njano) akipokea hati za makubaliano ya uanzishwaji wa Baraza Huru kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude (katikati).
Madiwani kutoka kata zinazozunguka Mgodi wa Almasi wa Mwadui, Kishapu Shinyanga kutoka kushoto ni diwani wa kata ya Maganzo, Lwizi Kidiga, Sarah Marco (kata ya Idukilo) na Abdul Ngoromole kata ya Songwa.
NiWajumbe wa Baraza Huru la kusilikiza malalamiko ya wananchi waliotendewa vya ukiukwaji wa Haki za kibinadamu wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi, mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude (wa tano kutoka kushoto walioketi kwenye viti). (Picha na Suleiman Abeid)