Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kujenga barabara ya kutoka Ruangwa hadi Kiranjeranje kwa kiwango cha lami.
Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa vijiji na kata mbalimbali za wilaya ya Ruangwa ambako alipita kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli na Madiwani wote wa kata hizo.
Amesema, barabara hiyo ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na tayari Sh. bilioni 1.2 zimeshatolewa ili kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara hiyo itakayowafanya wakazi hao wasilazimike kupitia Nanganga hadi Lindi wanapotaka kwenda Dar es Salaam.
“Barabara ya kutoka Ruangwa – Nanjilinji – Kiranjeranje ina urefu wa kilometa 120 na ukiangalia kwenye ilani yetu, utaikuta iko ukurasa wa 75. Barabara nyingine ni ya kutoka Ngongo – Mandawa – Namichiga yenye urefu wa km 85 na hii ilipatiwa sh. milioni 800 na kazi ya upembuzi yakinifu imekwishakamilika, sasa kazi iliyobaki ni kutafuta fedha na kuanza ujenzi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Majaliwa ambaye ni mbunge mteule wa jimbo la Ruangwa, amesema katika kipindi cha miaka mitano, wilaya hiyo imepokea zaidi ya sh. bilioni 100 kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
“Haijawahi kutokea tangu Wilaya hii ianzishwe mwaka 1995, imekuwa ikipokea fedha za maendeleo kati ya Sh. bilioni 3 hadi bilioni 4 lakini awamu hii tumepokea Sh. bilioni 49.5 kwa ajili ya kazi za maendeleo na hivi karibuni Dkt. Magufuli alitoa Sh. bilioni 59 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nanganga- Ruangwa kwa kiwango cha lami.”
Katika vijiji vyote alivyosimama na kata za Mandawa, Chikundi, Namichiga na Mbekenyera, Majaliwa amewasihi wakazi hao kuwa ifikapo Jumatano ijayo wajitokeze kwa wingi na kupiga kura za ndiyo kwa Dkt. Magufuli na madiwani wa CCM.
“Sisi sote ni wana-Ruangwa na kikubwa tunachotaka ni maendeleo, na maendeleo hayachagui chama. Kwani tukijenga barabara, si tutatumia wote? Fanyeni maamuzi sahihi kwa kukichagua Chama cha Mapinduzi na kumpa kura nyingi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,” amesisitiza.
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo