January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bandari ya Tanga yatoa elimu

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Tanga

KAIMU Meneja wa Bandari ya Tanga, Donald Ngaile amesema, wametumia maonyesho ya nane ya biashara yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mwahako jijini Tanga ili kuelezea huduma wanazozitoa kwa wananchi kwa sababu lengo la bandari ni kurahisisha biashara.

Ngaile ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao ambapo amesema wanarahisisha biashara kwa kupakua mizigo inayoingia na kupakia inayosafirishwa nje, hivyo huduma zao zinaathiri moja kwa moja maisha ya wananchi zinapokuwa bora zile bidhaa zinazopakulia mwisho gharama zikiwa kubwa za Bandari zinakwenda kuwaathiri wananchi.

Amesema, kwenye maonyesho hayo wamewaeleza kwamba bandari ya Tanga inafanya nini katika kurahisisha biashara na watawaeleza wananchi wa Tanga Bandari inafanya nini katika kurahisisha biashara na kuongeza thamani ya ubora wa huduma.

Amesema, ubora wa huduma ambazo zinatolewa lazima kuwe na vitendea kazi vya kutosha na bora kwa kuhakikisha meli inapokuja bandarini lazima ikae muda mfupi kwa sababu ikikaa muda mrefu inaonyesha kwamba hiyo bandari haina ufanisi.

Amesema, kipimo cha bandari yoyote Duniani ni ufanisi na kiasi gani mzigo unapakulia kwa saa na kiasi gani cha muda unamuhudumia mteja anapokuja kufuata huduma bandarini.

“Lakini unaweza kushindwa kutoa huduma bora kama vifaa ulivyonavyo vinaharibika mara kwa mara na hivyo kujikuta ukishindwa kufikia malengo uliojiwekea,”amesema.

Hata hivyo, amesema katika mwaka uliopita 2019/2020 walihudumia tani 569,270 za shehena na mwaka huu ndani ya miezi sita wamehudumia tani 349,205 na hivi sasa wameanza kupata shehena inayosafirishwa kwenda nchi jirani inayotumika kutengeneza saruji.