November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi wa shina atuhumiwa kuwakata vidole vya miguu vijana wawili wa familia moja

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline, Songwe.

BALOZI wa Shina namba 10 Mji Mwema, Samuel Mtambo, Mkazi wa Mtaa wa Nasele katika kata ya Mpemba, Wilayani Momba, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe akituhumiwa kuwakata vidole vya miguu vijana wawili wa familia moja baada ya kuwakamata na vipisi 17 vya Nondo vinavyodaiwa kuviiba kwenye moja ya nyumba katika mtaa wa balozi huyo.

Mtuhumiwa huyo na wenzake wawili ambao wanaendelea kutafutwa na jeshi hilo, wanadaiwa kuwakata vidole vijana hao wawili wa familia ambao ni Zefania Mdollo (20) na Kelvin Mdollo (17) kwa kutumia Msumeno unaodaiwa kutumiwa na vijana hao kukatia vipande vya nondo wanazotuhumiwa kuiba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya, akizungumza na waandishi wa habari Disemba 7, 2023, amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kufanya tukio hilo la ukatili alilolitenda kwa kushirikiana na wenzake hao wawili  Novemba 3, 2023.

“Inasemekana kwamba vijana hawa ambao ni ndugu walifika kwenye nyumba ambayo inajengwa na tayari imewekwa ‘Gril’ na kuanza kukata vipande vya nondo ndipo walipokamatwa na mtuhumiwa (Balozi) akiwa na wenzake wawili na kuchukua msumeno uliotumiwa na vijana hao na kuwakata vidole vya miguu” amefafanua Kamanda Mallya.

Kamanda Mallya amesema, kijana Zefania yeye alijeruhiwa kwa kukatwa kidole kikubwa cha mguu wa kushoto, huku mdogo wake naye alikatwa kidole cha mguu wa kulia na kwamba vijana hao baada ya kutendewa tukio hilo walienda kutoa taarifa kituo cha polisi Mpemba kwa kuandikisha majina ya uongo wakihofia kitendo walichokamatwa nacho kuiba Nondo.

Amesema baada ya kutoa taarifa kituo cha polisi na kupatiwa fomu namba 3 kwa ajili ya matibabu vijana hao hawakwenda kupatiwa matibabu Hospitalini badala yake waliendelea kujiuguza kwa kificho hadi jeshi hilo lilipopata taarifa na kufanikiwa kumkata mtuhumiwa.
Aidha, Kamanda Mallya alisema baada ya vijana hao kupatika hivi sasa wanaendelea kupatiwa matibabu kwa usimamizi wa jeshi hilo.