Na Mwandishi wetu timesmajira
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi ametoa wito kwa jamii ya Kitanzania kuendelea na jitihada zake za kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali za maisha, ili kuharakisha kasi ya maendeleo ya taifa.
Katika salaam zake za heri kwa wanawake wote, katika kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, inayoadhimishwa tarehe 8, Machi, kila mwaka, Balozi Nchimbi, akirejea kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu 2024, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa wanawake ili kuharakisha maendeleo na ustawi wa jamii kwa taifa.
“Kama kauli mbiu yetu yam waka huu inavyosema Wekeza kwa Wanawake: Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii, inatuhimiza umuhimu wa kuwawezesha wanawake katika jamii yetu, kiuchumi, kielimu, na kisiasa ili kuchangia kasi ya maendeleo ya Taifa na kuboresha ustawi wa jamii kwa ujumla. Nasi kwa upande wetu chama, tunajivunia kuwa mfano mzuri, kwa kuishi na kaulimbiu hii kwa kuwa na mifumo imara katika kutambua nafasi za wanawake na vipawa mbalimbali walivyonavyo,” amesema Balozi Nchimbi katika salaamu zake hizo.
Aidha, Balozi Nchimbi ametumia fursa hiyo kuungana na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan kuwatakia wanawake wote Heri ya Siku ya Wanawake Duniani, huku akitambua mchango mkubwa wa wanawake katika kujenga ustawi wa jamii nzima na watu wake.
Balozi Nchimbi ameongeza kuwa, CCM kama chama tawala, chenye dhamana ya kutoa uongozi wa nchi, kinajivunia na kutambua mchango wa viongozi mahiri na shupavu ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT).
“Kipekee, tunajivunia jumuiya yetu ya UWT inayoongozwa na Ndugu Mary Chatanda. Kwa hakika jumuiya hii iliyoasisiwa na Hayati Bibi Titi Mohamed kwa kiasi kikubwa imechangia kuandaa viongozi mahiri wa nchi hii. Viongozi kama Bibi Titi Mohamed, Mwanamajumui wa Afrika na Sofia Kawawa ni mojawapo ya matunda ya taasisi hii,” amesema Balozi Nchimbi.
Katibu Mkuu Balozi Nchimbi amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi, katika misingi hiyo ya kuwa na dhamana ya uongozi wa nchi, kitaendelea kuhakikisha kuwa wanawake wanapata fursa sawa katika nyanja zote za maisha, ikiwemo elimu, afya, ajira, uongozi, na maamuzi, huku akisisitiza kwamba kuwawezesha wanawake kiuchumi, kisiasa na kijamii ni jambo muhimu katika kuboresha ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Vilevile, kwa kwa niaba ya CCM, Balozi Nchimbi amewashukuru na kuwapongeza wanawake wote wanaojitolea na kuendelea kusaidia CCM katika ngazi zote za uongozi.
“Hakika, uimara wa chama chetu unatokana na kujitoa kwenu wanawake, kukipigania, kukitetea na kukisemea Chama na viongozi wake. Tunatambua mchango wenu na tunatambua kazi nzuri mnayofanya. Kwa dhati ya moyo wangu, nawashukuru sana na kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuhakikisha CCM inazidi kusonga mbele na kuendelea kuaminiwa,” amesema Balozi Nchimbi.
Balozi Nchimbi amehitimisha kwa kusisitiza kuwa CCM itaendelea kusimamia na kuhakikisha ustawi wa wanawake unaimarika ili kuwapa nguvu na uwezo katika kuchangia maendeleo ya taifa na jamii nzima kwa ujumla
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi