Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline,Zimbabwe
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi, amesema kuwa Watanzania wote kwa ujumla wao wanajivunia uwezo aliouonesha Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka 3 ya uongozi wake.
Aidha, amesema Rais Samia, amejidhihirisha kwa namna anavyoiongoza nchi, kwa ajili ya maendeleo ya watu, ustawi wa jamii na kuimarisha utaifa nchini.
Akizungumza mbele ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 11 wa Makatibu Wakuu wa Vyama Rafiki vya Ukombozi wa Kusini, unaoendelea katika siku yake ya pili, kwenye Mji wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe, juzi, Machi 19, 2024, Balozi Dkt. Nchimbi, alisema Chama Cha Mapinduzi pia kinajivunia uongozi wa Rais Samia, kwa jinsi anavyoendelea kuiongoza Serikali katika kutafsiri kwa vitendo utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025, akisisitiza kuwa CCM na wanaCCM wanamuunga mkono bega kwa bega.
“Kabla sijaanza kuwasilisha hapa kwa ruhusa yako Mwenyekiti wa Kikao, imekuwa kama bahati nzuri zilizogongana leo, naomba niwataarifu Wajumbe wa Mkutano wa 11 wa Makatibu Wakuu wa Vyama vya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika kwamba leo (Machi 19) ni maadhimisho ya mwaka wa tatu tangu Rais Samia aliposhika madaraka ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa kweli ninajivunia sana Rais Samia, si kwa sababu tu mimi ni mpigania haki za wanawake, bali kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa uongozi mzuri anavyoendelea kuiongoza nchi yetu ya Tanzania.
Kutokana na hilo, Chama Cha Mapinduzi kinajivunia sana uongozi wa Rais Samia , na Watanzania kwa ujumla wetu tunajivunia sana kuongozwa na Rais Samia kwa uwezo wake mkubwa ambao ameuonesha ndani ya hii miaka mitatu,” alisema Balozi Dk. Nchimbi.
Balozi Nchimbi pia alitumia nafasi hiyo kuwahakikishia wajumbe kuwa kutokana na kuwa mwanamajumuiya wa kweli wa Afrika, Rais Samia ana dhamira ya dhati kuimarisha na kuboresha uhusiano wa nchi na vyama rafiki katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na kwamba anafuatilia mkutano huo wa 11 wa Makatibu Wakuu wa vyama hivyo kwa ukaribu.
Aliwaomba wajumbe kuungana naye kumtakia kila la heri Rais Samia na kumuunga mkono, ombi ambalo lilipokelewa na kukubaliwa na wajumbe.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato