December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi Nchimbi aongoza ujumbe wa CCM ziarani China

Balozi Nchimbi aongoza ujumbe wa CCM ziarani China

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, anaongoza ujumbe wa viongozi wa (CCM) katika ziara rasmi inayofanyika nchini China, iliyoanza leo Agosti 23 hadi 31, 2024, kufuatia mwaliko wa Chama cha Kikomunisti cha nchini China (CPC).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM (SUKI), imeelezwa lengo la ziara hiyo ni kuendeleza na kuimarisha uhusiano wa kindugu na kihistoria, kati ya vyama vya CCM na CPC.

Pia, imeelezwa kuwa, ziara hiyo inalenga zaidi kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China, ambao umezidi zaidi ya miongo sita mwanzoni mwa mwaka 1960 wakati Tanzania ikipigania uhuru, ambapo uhusiano huo imeendelea kukua na kuimarika hadi sasa.

Katika ziara hiyo, mazungumzo baina ya Katibu Mkuu huyo, Balozi Dkt. Nchimbi na viongozi waandamizi wa CPC, yatajikita katika kubadilishana uzoefu wa kiuongozi na mikakati ya maendeleo, hususani katika masuala ya uchumi, elimu na teknolojia.
Aidha, ziara hiyo inatoa nafasi kwa Tanzania kuendelea kujifunza na kunufaika na uzoefu wa China katika kuendesha miradi mikubwa ya maendeleo, hasa ikizingatiwa kuwa China imekuwa mashirika wa karibu wa Tanzania katika miradi ya miundombinu, kilimo na viwanda.