December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi Mulamula awasili nchini Finland kwa ziara

Na Mwandishi wetu,timesmajira, Dar es Salaam

WAZIRI  wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Liberata Mulamula amewasili nchini Finland kwa ziara ya siku tatu
kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na
Nchi za Nordic (NORDIC-AFRICA) unaofanyika kuanzia juni 13 hadi
15,2022 jijini Helsinki, Finland.

Akifungua mkutano huo,Waziri wa Mambo ya Nje wa
Finland,Pekka Haavisto,amesema umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kujiletea maendeleo baina ya nchi hizo marafiki.

Amesema  mkutano huu utahusisha nchi tano  za Nordic ambazo ni Finland
mwenyeji wa mkutano  huo,Sweden, Norway, Iceland na Denmark
na nchi za Afrika 25 marafiki wa Nordic ikiwemo nchi ya Tanzania.

Pia amesema katika mkutano huo wa Mawaziri wa Mambo ya Nje utahusisha Mabalozi wa nchi shiriki za Afrika zinazowakilisha katika nchi za Nordic na
Mabalozi wa nchi za Nordic wanaowakilisha katika Nchi shiriki za
Afrika.

“Wazo la kuanzisha mkutano huu lilianza mwaka 2000 ambapo
mkutano wa kwanza ulifanyika nchini Sweden mwaka 2001 baada ya
hapo mikutano kama hii inafanyika kwa kupokezana kutoka Bara la
Afrika na upande wa Nordic,”amesema na kuongeza
“Mwaka 2019 Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano huu ambapo nchi
takribani 34 zilishiriki katika mkutano,”amesema

Wakati huo huo, Waziri Mulamula alitumia fursa ya ziara hiyo
kutembelea Makao Makuu ya Ofisi ya Mpango wa usimamizi wa
migogoro nchini Finland na kukutana na uongozi wa mpango huo lengo
likiwa kujadili masuala ya amani na usalama katika ukanda
wa Afrika Mashariki na ukanda wa kusini mwa Afrika.

Katika mazungumzo yake Waziri Mulamula ameeleza kuwa Tanzania
inaendelea kuwa mstari wa mbele katika kusimamia masuala ya amani
na usalama ili kuwezesha nchi za ukanda huo kufanya shughuli za
kiuchumi na kuinua maendeleo ya taifa na wananchi kwa ujumla.